Habari
MHE. REGINA QWARAY AFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS MSTAAFU MHE. JAKAYA KIKWETE
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Regina Qwaray amtembelea na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete nyumbani kwake Kawe Dar es Salaam tarehe 19 Februari 2026.
“Rais, amenielekeza kuwafikishia salaam zake na amesema yuko pamoja nanyi na ndio mana amenituma kufika hapa nyumbani na kukujulia hali, kusikiliza changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi” amesema Mhe. Qwaray.
Mhe. Qwaray amesema Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anathamini sana mchango wa Viongozi Wakuu wa Kitaifa waliomtangulia na ataendelea kusimamia na kutunza familia hizo kwa mujibu wa Katiba na Sheria.
Aidha, Mhe. Kikwete amemshukuru Mhe. Qwaray kwa kupata nafasi ya kumtembelea na kumjulia hali na ametumia fursa ya mazungumzo yao kumpongeza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa wakati wote bila kuchoka na amemuombea dua ili aendelee kutumia hekima na busara katika kuiongoza Tanzania.
