Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MHE. QWARAY ASISITIZA UTUNZWAJI MIRADI YA TASAF


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe Regina Qwaray amesisitiza waratibu wa miradi ya TASAF kwa kushirikiana na kaya nufaika kulinda miradi dhidi ya waharifu wa miundombinu hiyo ili iweze kutumika kwa manufaa ya walengwa na taifa kwa jumla.

Mhe. Qwaray ameyasema hayo leo Januari 9, 2026 alipokuwa akizungumza na waratibu, wasimamizi na wanufaika wa miradi ya TASAF Mkoani Arusha.

Mhe. Qwaray amewapongeza TASAF kwa taarifa nzuri ya ujenzi wa shule ya sekondari Oldonuwas iliyopo kijiji cha Oldonuwas na ujenzi wa mfereji wa umwagiliaji uliopo Meru kijiji cha Ngabobo wilaya ya Meru.

“Nimesikiliza taarifa zenu na nimejionea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo yenye manufaa kwa wanufaika wa TASAF na taifa kwa jumla, hivyo nitoe rai ya kuilinda na kuithamini ili tupate tija iiyokusudiwa na Serikali” alisema Mhe. Qwaray.

Aliongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi ili kuhakikisha watanzania hasa kaya maskini zinanufaika kupitia TASAF. Hivyo, amewaomba wananchi wa wanaozunguka miradi hiyo kuwa walinzi ili miradi hiyo iweze kunufaisha vizazi vya sasa na vile  vijavyo.

Aidha, Mhe. Qwaray amesema kuwa miradi ya TASAF ni chachu ya maendeleo kwa kuwa watanzania hasa wanaotoka katika kaya maskini wanajikwamua kutoka katika wimbi la umaskini kwa kupata elimu kutokana na ujenzi wa shule na wananufaika na mfereji wa umwagiliaji kwa kufanya kilimo cha mahindi, nyanya, vitunguu na maji kwa ajili ya mifugo.