Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MHE. KIKWETE ASISITIZA WATUMISHI WA UMMA KUSHUGHULIKIA HOJA NA MALALAMIKO YA WANANCHI KWA WAKATI


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewasisitiza watumishi wa umma kushughulikia hoja na malalamiko ya wananchi kwa wakati  ili kuwapunguzia Viongozi wa Kitaifa adha ya kushughulikia masuala ambayo yangeweza kumalizwa katika vituo vya kutolea huduma.

“Sote tumeshuhudia namna ambavyo kunakuwa na mabango yenye malalamiko wakati wa ziara za Viongozi wa Kitaifa. Hii inaashiria kuwa watendaji wetu katika vituo vya kazi hawatekelezi majukumu yao ipasavyo na hivyo kusababisha wateja kutafuta suluhisho sehemu nyingine” amesisitiza

Mhe. Ridhiwani amesema hayo wakati akifunga kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora kilichowashirikisha wadau kutoka Taasisi Simamizi za Maadili ya Utendaji, Taasisi Simamizi za Maadili ya Kitaaluma na watumishi kutoka kwenye Wizara mbalimbali na taasisi za kitaaluma katika ukumbi wa PSSSF-Makole Dodoma.

Aidha, Mhe.Ridhiwani ametoa rai kwa washiriki hao kufanyia kazi kwa vitendo masuala waliyojifunza katika siku hizo mbili ili kuendana na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na Watumishi wa Umma ambao ni Waadilifu na wenye kuwajibika kwa hiari.

Ameongeza kuwa wataalamu wa ofisi yake kwa kushirikiana na Taasisi Simamizi za Maadili katika Utumishi wa Umma wanafanyia kazi hoja na changamoto mbalimbali kuhusu usimamizi wa maadili, nidhamu na michakato ya ajira ili kuondoa malalamiko yaliyopo na kuleta ufanisi zaidi.

Naye, Kaimu Katibu Mkuu Bi. Leila Mavika amesema Ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora itaendelea kushirikiana na wadau kutoka Taasisi Simamizi za Maadili ya Utendaji, Taasisi Simamizi za Maadili ya Kitaaluma na watumishi kutoka kwenye Wizara mbalimbali na taasisi za kitaaluma kutoa ushauri wa kitaalamu pale itakapohitajika, kujenga uelewa kuhusu maadili ya Utumishi wa Umma na kushirikiana na wadau hao kuleta mabadiliko ya fikra miongoni mwa watumishi wa umma.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma Bi. Jane Mazigo ameishukuru ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora kwa kuandaa mafunzo haya muhimu kwa wadau kutoka Taasisi Simamizi za Maadili ya Utendaji, Taasisi Simamizi za Maadili ya Kitaaluma na watumishi kutoka kwenye Wizara mbalimbali na taasisi za kitaaluma.

“Mhe. Naibu waziri tumejifunza mambo mengi na tuko tayari kuelimisha kundi kubwa la watumishi wa umma kuzingatia masuala ya nidhamu na Uadilifu kazini. Kundi hili limejifunza masuala muhimu na kwa watu muhimu na sisi hatutokuangusha” alisisitiza