Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MHE. KIKWETE ASEMA USHIRIKIANO UTABORESHA OFISI YA NYARAKA ZANZIBAR


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewahakikishia Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi  Zanzibar  kuwa    Idara ya  Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa   ipo tayari kushirikiana na Ofisi ya Nyaraka Zanzibar kuhakikisha inaboreshwa kwa maslahi ya pande zote mbili  za Muungano.

Mhe. Kikwete ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Desemba 12, 2023 wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati hiyo walipotembelea ofisi za Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Kanda ya Mashariki zilizopo Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Kikwete ameeleza lengo la ziara ya Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi  Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi  Zanzibar kwenye ofisi za Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dar es Salaam ni kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna ya kutunza na kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu za Taifa kwa maslahi ya vizazi vijavyo.

 “Tupo tayari kushirikiana nanyi ili kuhakikisha kumbukumbu na nyaraka za Waasisi wa Taifa letu zinalindwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kutusaidia kufanya uamuzi wenye mwelekeo sahihi na kulinda maslahi ya  kizazi cha sasa na cha baadaye’’ amesisitiza Mhe. Kikwete

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu, Jamal Kassim Ali ameiomba Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kuunga mkono jitihada mbalimbali zitakazofanywa na Ofisi ya Nyaraka Zanzibar kwa lengo la kuiboresha na kuhakikisha kumbukumbu na Nyaraka za Viongozi Wakuu wa Zanzibar zinatunzwa na kuhifadhiwa kwa maslahi mapana ya Taifa.

“Ofisi yetu ni changa na hivi karibuni tutasherehekea miaka 60 ya mapinduzi, hivyo tuomba ushirikiano wenu wa namna bora ya kutunza kumbukumbu za viongozi mbalimbali hususani kumbukumbu za Hayati Abeid Aman Karume” alisema Mhe. Jamal Kassim Ali.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Machano Othman Said amesema kuwa utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za taifa ni shughuli muhimu sana katika maendeleo ya nchi. Hivyo,

Mhe. Machano ameisihi Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kuwa tayari kutoa elimu, vifaa na uzoefu wa namna bora ya kutumia teknolojia katika uendeshaji wa  Ofisi ya Nyaraka Zanzibar.