Habari
MHE. KIKWETE AIELEKEZA TASAF KUFANYA TATHMINI NA UFUATILIAJI WA SHUGHULI ZA MPANGO ILI KUONA NI KWA KIWANGO GANI MALENGO YA MPANGO YANAFIKIWA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameielekeza Menejimenti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kufanya tathmini na ufuatiliaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili kuona ni kwa kiwango gani malengo ya Mpango huo yanafikiwa, kubainisha changamoto na kuzishughulikia ili kuboresha utendaji kazi na matokeo yanayotarajiwa.
Mhe. Kikwete ameyasema hayo leo tarehe 05 Disemba, 2025 alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya TASAF wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa TASAF jijini Dar es Salaam.
Amesema kufanya tathmini kutafichua mambo mengi ambayo yalikuwa hayajulikani katika utekelezaji ambapo itasaidia kuboresha awamu nyingine ya Mpango. “Tufanye tathmini tuangalie kwanini kunakuwa na utofauti katika mafanikio ili tuone tunasaidiaje, je wasimamizi wa eneo fulani wana ubunifu zaidi kuliko wa eneo lingine? Amejiuliza, na kuongeza kuwa haya mambo ni vizuri yakawa shirikishi ili kuboresha zaidi tutakapoingia kwenye awamu nyingine ya Mpango,” Mhe. Kikwete ameongeza
Aidha, ameitaka TASAF kuzungumza mafanikio na changamoto za utekelezaji wa mradi huo kwa walengwa na wananchi. “Tutoke, tuseme mafanikio na changamoto kwanini wamekosa, watu waambiwe ukweli, TASAF imefanya mambo makubwa, tuwaonyeshe waliohitimu, wamefanya nini mpaka kufanikiwa na walioshindwa kufanikiwa wanatakiwa kufanya nini.” Mhe. Kikwete amesisitiza.
Mhe. Kikwete ameipongeza taasisi hiyo kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa uendelea kuhawilisha ruzuku kwa kaya maskini zinazokidhi vigezo vya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye Sekta za Afya, Elimu, Maji, Mazingira na ujasiriamali.
Pamoja na pongezi hizo ameitaka TASAF kuendelea kuboresha shughuli za kuwezesha utekelezaji wa Miradi ya Jamii ya kutoa Ajira ya muda ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa Ajira, kuwezesha jamii kutekeleza miradi ya kuendeleza miundombinu ya huduma za jamii katika Sekta za Afya, Elimu, Maji, Mazingira na ujasiriamali na uendelea kufungamanisha mikakati mbalimbali ya kuwezesha wananchi kiuchumi ili kuhakikisha matokeo yanayopatika kwenye kila mkakati yanaharakisha kasi ya kuondoa umaskini wa wananchi.
Vile vile ameitaka Taasisi hiyo kuimarisha miundombinu ya mifumo ili kulinda usalama wa taarifa za walengwa na kuungamanisha mifumo wa walengwa na mifumo mingine ya Serikali pamoja na kuongeza idadi ya walengwa wanaolipwa kwa njia za kielektroniki ili kupunguza dosari za malipo ya ruzuku.
Mhe. Kikwete amesema malengo makubwa ya yeye na Naibu Waziri Mhe. Mhe. Regina Qwaray kutembelea TASAF leo ni kujitambulisha na kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufikia malengo ya TASAF yaliyokusudiwa.
“Mimi sio mgeni katika Ofisi hii, hivyo ninawaahidi tutaendelea kushirikiana kama ambavyo tulikuwa tukifanya siku zote nilipokuwa hapa kwa nafasi ya Naibu Waziri. Kuletwa kwangu katika Ofisi hii ni kuja kuongeza nguvu ili kupata matokeo chanya ikiwemo ubunifu katika maeneo mbalimbali. Tufanye kazi tuliyopangwa kufanya tukiongozwa na misingi yetu ya utendaji kazi. Lengo ni kujenga na kumsaidia Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupunguza kaya masikini katika taifa letu.
Pia Mhe. Kikwete amesema dhana ya ushirikishwaji wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ni nzuri kwani imewasaidia kubuni miradi mbalimbali na imepunguza changamoto nyingi ikiwemo za miundo mbinu, afya na elimu.
Amesisitiza kuwajengea uwezo wa kifikra walengwa, fedha ziwafikie kwa wakati, usimamizi mzuri huku wakitambua kuwa msingi mkubwa wa Mpango huo walengwa wake ni wananchi na si vinginevyo.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mhe. Regina Qwaray ameipongeza TASAF kwa kazi nzuri wanayoifanya. “Mimi ni mgeni katika Ofisi hii, lakini napenda niwapongeze kwa kazi nzuri mnayoifanya, TASAF sio ngeni masikioni mwangu, hii inaonyesha ni kwa jinsi gani mnatekeleza majukumu yenu vizuri, naombeni ushirikiano ili tufanye kazi kwa pamoja na kuwa na matokeo chanya,” amesema Mhe. Qwaray.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Shadrack Mziray amesema Mfuko huo ulianzishwa na Serikali mwaka 2000 kama mojawapo ya mikakati katika kupambana na umaskini kwa kutumia dhana ya ushirikishaji jamii na imetekelezwa kwa awamu tatu tangu kuanzishwa kwake.
