Habari
MFUMO WA USHUGHULIKIAJI WA RUFAA NA MALALAMIKO UTAONGEZA UFANISI KATIKA UTOAJI HAKI KWENYE UTUMISHI WA UMMA-Mhe. Sangu

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu amesema mafunzo yanayotolewa kwa Washiriki kutoka Serikali Kuu zikiwemo (Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Idara zinazojitegemea na Wakala za Serikali), Taasisi za Umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu Mfumo wa ushughulikiaji wa Rufaa na Malalamiko yataongeza ufanisi katika utoaji haki kwenye Utumishi wa Umma.
Mhe. Sangu amesema hayo leo wakati akifungua mafunzo ya Mfumo wa ushughulikiaji wa Rufaa na Malalamiko katika Utumishi wa Umma yanayofanyika Mkoani Morogoro.
Mhe. Sangu amesema kuwa, kutokana na Serikali kusisitiza matumizi ya mifumo kwenye utendaji wa shughuli zake, Tume ya Utumishi wa Umma, imejenga Mfumo wa kushughulikia Rufaa na Malalamiko kwa Watumishi wa Umma, Mamlaka za Rufaa, Mamlaka za Nidhamu na Waajiri kwa lengo la kutoa huduma bora ili kuendana na Serikali ya kidijitali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Sangu ameongeza kuwa mfumo huo utasaidia kupatikana kwa taarifa za hali ya Utumishi wa Umma kwa wakati na katika ubora unaotakiwa kulingana na uzito wa taarifa hizo.
Naibu Waziri Sangu amewasihi washiriki wa mafunzo hayo kutumia vyema Mfumo huo na kuhakikisha wanatuma taarifa sahihi Tume ya Utumishi wa Umma kwa lengo la kuchakatwa na kuwasilisha taarifa hizo kwa Mamlaka husika ili kuirahisishia Serikali kupanga masuala mbalimbali yanayohusu Utumishi wa Umma.
Aidha, Naibu Waziri Sangu amewataka Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu kuwasilisha vielelezo vya rufaa na malalamiko Tume ya Utumishi wa Umma kwa wakati kama Sheria inavyoelekeza pale zinapotakiwa kufanya hivyo.
Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma Mhe. Hamisa Kalombola (Jaji Mst), amesema kuwa Tume iliamua kujenga mifumo ya kielektroniki na kuendelea kutoa elimu ya kutumia mifumo hiyo kwa wadau wao ili kuondokana na baadhi ya changamoto ambazo zilikuwa zinakwamisha utendaji kazi wa namna ya kuitumia wakati wa uendeshaji wa mashauri na nidhamu hasa kwenye ushughulikiaji wa rufaa na malalamiko.
Awali, Kaimu Katibu, Tume ya Utumishi wa Umma Bw. John Mbisso alisema, mafunzo hayo yanafanyika ili kutekeleza Sheria ya Utumishi wa Umma ya kutoa miongozo na elimu ya masuala mbalimbali ya kiutumishi kwa lengo la kuboresha usimamizi wa Watumishi wa Umma.
Tume ya Utumishi wa Umma ni chombo rekebu chini ya Ofisi ya Rais kilichoundwa kwa mujibu wa Kifungu cha 9(1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 [Marejeo ya Mwaka 2019].
Aidha, majukumu ya Tume yameainishwa katika Kifungu cha 10(1) cha Sheria hiyo ambapo baadhi ya majukumu yake ni pamoja na kutoa Miongozo, Uwezeshaji, Utafiti, kufuatilia Uzingatiaji katika Usimamizi wa Utumishi wa Umma na ushughulikiaji wa Rufaa na Malalamiko katika Utumishi wa Umma.