Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MFUMO WA AJIRA WADUMISHA MUUNGANO WA TANZANIA


 

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kuweka utaratibu wa mgao wa ajira unaotekelezwa kwa mujibu wa Waraka wa Serikali wa tarehe 10 Mei, 2013 ambapo Tanzania Bara ni asilimia 79 na Tanzania Zanzibar ni asilimia 21.

 

Ameyasema hayo leo Aprili 15, 2024 jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya Muungano kwa upande wa Ofisi yake.

 

Amesema katika kipindi hicho cha miaka 60 ya Muungano, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na Tume ya Utumishi wa Umma Zanzibar inayoratibu masuala ya ajira katika watumishi wa umma ili kurahisisha zoezi la utangazaji wa nafasi za kazi na upatikanaji wa watumishi.

 

Kutokana na ukuaji wa teknolojia, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imesanifu na kujenga mfumo wa kidijitali wa ajira Serikalini ambao ni rafiki kwa watafuta fursa wote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Aidha, Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa utengenezaji wa programu ya rununu (Ajira Portal Mobile App) inayopatikana kwenye PlayStore na ApStore za simu janja inalenga kuimarisha Muungano kwa kuwarahisishia waombaji wa fursa za ajira kupata taarifa za uwepo wa fursa hizo kiganjani mwao mahali popote.

 

Katika hatua nyingine Mhe. Simbachawene amesema Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imedhamiria kuondoa changamoto zinazowakabili waombaji wa fursa za ajira Tanzania Bara na Zanzibar.

 

Aidha, matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kipindi hiki cha miaka 60 ya Muungano imesaidia waombaji kuepuka gharama za usafiri, malazi na changamoto za ajali, wakati Serikali imepunguza muda wa usaili na gharama za uendeshaji wa zoezi hilo.

 

Mhe. Simbachawene amewataka watafuta fursa za ajira wote kutoka pande mbili za Muungano kufahamu akaunti zao, nywila na kuwa mahiri katika matumizi ya kompyuta ili kuepukana na usumbufu.