Habari
MATUMIZI YA OFISI MTANDAO SERIKALINI NI LAZIMA-Mhe. Simbachawene
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewataka Wakuu wa Taasisi zote za Umma kutumia mfumo wa Ofisi Mtandao (e-office) katika utendaji kazi na kuachana na matumizi makubwa ya karatasi katika utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka.
Wito huo umetolewa leo Mei 9, 2024 wakati akifunga kikao kazi na mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji wanataaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania yaliyofanyika kwa muda siku nne kuanzia tarehe 6 hadi 9 Mei, 2024 Mjini Iringa.
Mhe. Simbachawene amesisitiza kuwa matumizi ya mfumo wa ofisi mtandao katika utendaji kazi sio hiari wala ombi tena bali ni maagizo ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anayetaka kuona tija zaidi katika utendaji kazi wa Serikali kwa kuwa na Serikali ya Kidijitali.
“Waajiri walio wengi Serikalini hawachangamkii matumizi ya mfumo wa e-office, na badala yake wamekuwa wakiendelea kutumia karatasi zaidi na makabati ambayo hata hivyo, hayazingatii utaratibu wa utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za Serikali.
Ameongeza kuwa, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wataalamu wa menejimenti ya kumbukumbu na nyaraka kwa usalama na ustawi wa taifa. Aidha, amewafahamisha washiriki hao kutambua kuwa Serikali imewaamini na kuwapa dhamana kubwa ya kutunza kumbukumbu na nyaraka zake muhimu, kwa hiyo hawana budi kulinda dhamana hiyo na kuitendea haki kwa ustawi na maendeleo ya taifa.
Amesisitiza kuwa kwa yeyote atayebainika kutoa au kuvujisha siri za Serikali atachukuliwa hatua za kinidhamu na kuwajibishwa kwa mujibu wa Taratibu, Kanuni na Miongozo ya kiutumishi.
Amewapongeza waajiri waliowaruhusu maafisa kushiriki kikao kazi na mafunzo hayo maalumu na kuwalipa posho ya kujikimu na nauli. Vilevile ametumia fursa hiyo kuwalaumu waajiri waliowazuia watumishi wa kada hiyo kushiriki kikao kazi hicho ambacho ni utekelezaji wa sehemu ya maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyotoa wakati wa kikao kilichofanyika Zanzibar.
Kikao kazi na mafunzo maalumu hayo yamewakutanisha wanataaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania takribani 1500 kutoka taasisi mbalimbali za umma Tanzania Bara na Visiwani chini ya kaulimbiu isemayo “Misingi bora ya Utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, Uadilifu na utunzaji siri ni nguzo ya kitaaluma”.