Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MARUFUKU HUJUMA BAINA YA WATUMISHI MAHALI PA KAZI


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – UTUMISHI na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Bw. Juma Mkomi amewataka Watumishi katika ofisi yake kupendana na kuthaminiana mahali pa kazi huku akiwasihi kuacha tabia ya kuhujumiana.

Ametoa kauli hiyo leo Machi 26, 2024 Jijini Dodoma wakati akifungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala  Bora kilichowakutanisha Watumishi hao pamoja na baadhi ya Wajumbe wa TUGHE Taifa.

"Sisi ni jicho katika Utumishi wa Umma tujitahidi kufanya kazi kwa kushirikiana na kuheshimiana ili kutimiza malengo tuliyojiwekea ikiwa ni pamoja na kutoa huduma kwa watumishi na wananchi kwa jumla kwa haraka na kwa ufanisi " amesisitiza Mkomi.

Bw. Mkomi amewataka watumishi hao kupendana kwa kuwa sehemu kubwa ya muda wao unatumika kazini. Hivyo, mazingira ya kazi yanatakiwa kuwa na amani na utulivu ili ufanisi uongezeke na mwananchi aweze kupata huduma bora.

Vilevile, ametoa wito kwa Wakurugenzi wote kuwaandaa watumishi walio chini yao kwa ajili ya kurithishana madaraka na kuwapa majukumu watumishi hao ili kuwajengea uwezo kiutendaji na kuwafanya waoneshe uwezo wao kazini.

Aidha, Katibu Mkuu Mkomi amewanyooshea vidole baadhi ya watumishi wenye tabia ya kuvujisha siri ambapo amewatahadharisha kuwa yeyote atakayebainika hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.

Naye, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, TUGHE Bw. Nsubisi Mwasandende ametumia fursa ya mkutano huo kuwaomba Wakurugenzi wa Idara na Vitengo kuwasikiliza watumishi walio chini yao kwa kuwa wanaweza kuwa na mawazo mazuri yenye kujenga taasisi na Serikali kwa jumla.