Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MAKAMU WA RAIS, PHILIP MPANGO KUZINDUA MPANGO WA MAKAZI YA WATUMISHI


 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Dkt. Philip Mpango, anatarajiwa kuzindua Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma Disemba 11, 2024 katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma wenye lengo la kutatua changamoto za makazi kwa Watumishi wa Umma nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amebainisha hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu uzinduzi wa Mpango huo.

Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma ulianza kutekelezwa mwaka 2014 chini ya usimamizi wa Watumishi Housing Investments (WHI) na hadi sasa, zaidi ya nyumba 1,000 zimejengwa katika mikoa 19 nchini Tanzania, ikiwemo Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Morogoro, Simiyu,  Mtwara,amesema Mhe. Senyamule

Aidha, amesema Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuboresha ustawi wa Watumishi wa Umma, kuhakikisha wanapata makazi bora, yenye gharama nafuu na salama.

Kupitia mpango huu, Watumishi wa Umma wanapata fursa ya kumiliki nyumba kwa masharti nafuu, hatua inayolenga kuboresha hali ya maisha na kuongeza ufanisi kazini.

Aidha mpango huu unalengo la kuwawezesha wananchi na hasa Watumishi wa Umma kiuchumi kupitia umiliki wa nyumba,amesema Mhe. Senyamule

Mhe. Senyamule ameongeza kuwa Watumishi Housing Investments kupitia mpango huo imetoa mikopo yenye masharti nafuu kwa Watumishi wa Umma ili kuwawezesha kumiliki nyumba kwa urahisi zaidi.

Utekelezaji wa Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma ni dhamira pana ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata fursa ya kumiliki makazi bora,amesisitiza

Amesema Ofisi ya Rais,  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, inawaalika Watanzania wote kushiriki katika hafla hiyo muhimu ambayo inaashiria hatua kubwa katika kuboresha maisha ya Watumishi wa Umma na maendeleo ya sekta ya makazi nchini.

Hafla hii si tu uzinduzi wa Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma, bali pia ni fursa ya kuonyesha mshikamano wa kitaifa katika kutatua changamoto za makazi na kuimarisha ustawi wa jamii,amesema Mhe. Senyamule.