Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MAAFISA MASUULI WATAKIWA KUZINGATIA USHAURI WA WATAALAMU KATIKA TAASISI ZAO


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewataka Maafisa Rasilimaliwatu na Maafisa Sheria kutoka katika Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya kutoa ushauri mahususi kwa Maafisa Masuuli wao ili kuepuka kuipa hasara Serikali.

“Ninajua kusimamia rasilimaliwatu sio jambo jepesi kwani linahitaji hekima na busara. Wapo baadhi ya Maafisa Masuuli ambao hawasikilizi na hawapendi kupokea ushauri wa kitaalamu  kutoka kwa maofisa wao na hivyo kutoa uamuzi kinyume na matakwa ya sheria na kanuni za Utumishi wa Umma, hivyo kuipa hasara Serikali” amesema Mhe. Simbachawene.

Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa, iwapo sheria na kanuni za usimamizi wa rasilimaliwatu katika utumishi wa umma hautazingatiwa, utaondoa adhima ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na utumishi wa umma unaotenda haki na wenye kuwajibika kwa umma.

Aidha, amebainisha kuwa, taasisi za umma zinapokuwa na malalamiko mengi ya watumishi ni ishara kuwa watendaji wa ofisi hizo hawafanyi kazi ipasavyo hata kama lalamiko liko ndani ya uwezo wao. Hivyo, kitendo cha kupeleka malalamiko hayo katika ngazi za juu kwa utatuzi ni dhihaka kwa utawala.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Bw. Juma Mkomi amesema Maofisa hao ni washauri wakuu wa Maafisa Masuuli katika taasisi zao, hivyo wanatakiwa kutoa ushauri kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ili kuepuka kuumiza watumishi.

Bw. Mkomi amewasihi maofisa hao kuhakikisha wanatatua matatizo ya watumishi wa umma kwa kuwasikiliza na wakati mwingine kuwaonya kwanza kuliko kuwafukuza katika utumishi wa umma jambo.

Awali, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria katika Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bi. Hilda Kabissa amesema kikao kazi hiki kimelenga kuwajengea uwezo Maafisa Rasilimaliwatu na Maafisa Sheria katika kutekeleza Sheria, Kanuni na Miongozo ya Utumishi wa Umma.

Amesema, anaamini mada zilizowasilishwa zimeeleka kwa vizuri na washiriki wameahidi kuzifanyia kazi mafunzo haya kwa umahiri mkubwa sana na kuhakikisha wanahimiza haki na wajibu kwa watumishi wa umma.

Ameongeza kuwa maofisa hao pamoja na mambo mengine wamepitishwa katika masuala ya maslahi ya watumishi, uzingatiaji wa maadili mahala pa kazi, mifumo ya TEHAMA Serikalini, kutambua mifumo ya upimaji wa utendaji kazi Serikalini, utaratibu wa kuendesha mashauri ya kinidhamu katika utumishi wa umma.