Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MHE. RIDHIWANI KIKWETE; MAADILI NI MSINGI WA MAGEUZI YA MAENDELEO ENDELEVU


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewasisitiza watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na ubunifu ili tija ya kazi zao iweze kuonekana kupitia huduma bora wanazozitoa kwa wananchi.

“Ninatamani kuona utendaji kazi wenu unazingitia misingi ya maadili ya utendaji katika utumishi wa Umma kwani ndiyo msingi wa mageuzi kuelekea maendeleo endelevu vinginevyo watumishi wazembe na wenye mienendo isiyofaa kimaadili mwisho wao umefika.” alisisitiza Mhe. Ridhiwani.

Aidha, amewakumbusha watumishi hao kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anasisitiza uadilifu kazini na ametoa haki na stahiki mbalimbali kwa watumishi, hivyo, Serikali kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imekamilisha mapitio, kusanifu na kuanza kujenga mifumo ya utendaji kazi Serikalini ili dhana ya wajibu pia iweze kutekelezeka kwa ufanisi.

Pia, Naibu Waziri huyo amezitaka Mamlaka za Ajira na Nidhamu kuendelea kusimamia haki na stahiki zote za watumishi na kuachana na kasumba ya utendaji wa mazoea. Pia, amesema Mamlaka za Ajira na Nidhamu zirejee Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 ambayo inaonesha kuwa madaraka kuhusu ajira, kuthibitishwa kazini, mafunzo, kupandishwa cheo, nidhamu hadi hitimisho la kazi kwa mtumishi wa umma yalishagatuliwa na hivyo kushindwa kutekeleza wajibu huo ni kielelezo cha kushindwa kutekeleza majukumu waliyopewa.

Katika hatua nyingine Mhe. Ridhiwani amezitaka Halmashauri nchini kuhakikisha zinaendeleza miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF kwa kuwa ni chaguo na imeridhiwa na wananchi wenyewe katika maeneo yao. Iwapo Halmashauri na TASAF zitaunganisha nguvu ni rahisi kuwakomboa wananchi katika umaskini.

“Ninaelekeza walengwa wote wenye sifa za kunufaika na TASAF wasilipwe fedha nusu nusu kwa kuwa lengo ni kuwatoa katika wimbi la umaskini” alisema Mhe. Ridhiwani.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mhe. Kemilembe Lwotta ameomba pongezi zifike kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta watumishi wapya wa kada mbalimbali 228 na wote wameripoti kazini na watumishi 289 walimu na wasio walimu wamepandishwa vyeo na 15 wamebadilishiwa vyeo.

Vilevile, ameongeza kuwa wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi katika vijiji vyote 39 wananufaika vyema na uwepo wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF kwa kiwango kikubwa kwa kuwa kaya masikini zimefikiwa na zinawezeshwa kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi Bw. John Mgalula pamoja na shukurani alizotoa kwa Serikali, ameomba Serikali kuendelea kutoa vibali vya ajira ili watumishi waongezeke na utoaji huduma kwa umma uimarike.

Mhe. Ridhiwani amehitimisha ziara yake ya siku moja tarehe 25 Agosti, 2023 katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri  hiyo.