Habari
KIKWETE AFUNGUA PAREDI YA MIFUGO NA KITUO CHA HUDUMA KWA WATEJA NANENANE
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesisitiza wafugaji kuendelea kutumia mbinu bora za ufugaji katika kuongeza thamani ya mifugo ili kukidhi matakwa ya soko la ushindani wa mifugo ndani na nje ya nchi.
Mhe. Kikwete amebainisha hayo leo tarehe 5 Agosti, 2026 wakati akifungua Paredi ya Mifugo katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima maarufu kama Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa paredi hiyo, Mhe. Kikwete alisema kuwa sekta ya mifugo ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa kupitia uzalishaji, biashara na ajira. Hivyo, hatuna budi kuongeza juhudi na jitihada za kuimarisha mbinu za ufugaji bora kwa maslahi ya taifa.
Vile vile, Mhe. Kikwete aliwataka wadau wa sekta ya mifugo kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa sera na programu mbalimbali zinazolenga kuboresha huduma za ugani, udhibiti wa magonjwa ya mifugo na kuimarisha miundombinu ya masoko.
“Nitumie fursa kuwahamasisha wafugaji wote nchini kubadilisha mtazamo wa ufugaji wa kimazoea kwenda ufugaji unaotumia sayansi, takwimu na teknolojia na pia kushiriki na kuleta mifugo yao kwa ajili ya gwaride na mashindano kwa mwaka ujao 2027” alisema Kikwete.
Aidha, Paredi hiyo ilihusisha maonesho ya aina mbalimbali za mifugo ikiwemo ng'ombe, mbuzi na mifugo mingine ambapo wafugaji na taasisi mbalimbali walipata fursa ya kuonesha ubora wa mifugo yao pamoja na teknolojia na ubunifu unaotumika katika kuendeleza sekta hiyo.
Waziri Kikwete pia alitoa rai kwa taasisi za fedha nchini kuendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu na kubuni huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji ya wafugaji, hususan wanawake na vijana, ili waweze kuwekeza katika sekta hii.
Pamoja na ufunguzi wa paredi ya mifugo, Mhe. Kikwete amezindua rasmi kituo cha huduma kwa wateja cha Wizara ya Kilimo na Uvuvi ambacho kitakuwa mahususi kwa ajili ya kutoa nakupokea taarifa za Kilimo na Uvuvi.
Amewataka watumishi watakaokuwa katika kituo hicho kupokea na kujibu hoja za wakulima, wafugaji na wavuvi kwa wakati ili kurahisisha zoezi la uzalishaji na uuzaji wa bidhaa za kilimo.
