Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

KATIBU MKUU – UTUMISHI, BW. JUMA MKOMI AISHUKURU BENKI YA NMB KWA KUTOA ELIMU YA MASUALA YA KIFEDHA KWA WATUMISHI


Na Eric Amani -Dodoma

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi ameishukuru timu ya wawezeshaji kutoka Benki ya NMB Dodoma kwa kufika katika Ofisi za Utumishi kwa ajili ya kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali yanayohusiana na huduma za kibenki kwa watumishi wa Ofisi hiyo.

Bw. Mkomi amesema hayo leo Jumatatu Agosti 11, 2025 katika Ofisi za Utumishi jijini Dodoma, wakati wa mafunzo kwa watumishi wa Ofisi hiyo ikiwa ni utaratibu wa kila siku ya Jumatatu ya wiki ambapo Watumishi wa Ofisi hiyo hupewa  mafunzo mbalimbali kwa lengo la kuboresha utendaji kazi.

Baada ya kupata elimu hiyo ya masuala ya fedha, Katibu Mkuu Mkomi amewasisitiza watumishi wa Ofisi yake kujenga utaratibu wa kujiwekea akiba pamoja na kukata bima za mali zao ili wanapopata majanga ya mali hizo wasichanganyikiwe.

“Nawashukuru sana NMB kwa elimu nzuri ya masuala ya fedha hususan kuhusu ukataji wa bima ya mali tulizo nazo na kusema kuwa nina hakika wengi wetu hapa hatujakata bima ya nyumba zetu wakati tumejenga nyumba zenye thamani, tunakimbilia kuweka bima ya magari pekee, na kuongeza kuwa, elimu tuliyoipata hapa itusaidie kutekeleza haya tuliyofundishwa kwa mustabali wa maisha yetu na ya watoto wetu.

Awali, Meneja wa Benki ya  NMB tawi la Dodoma,  Bw. Amos Daniel  amewashauri Watumishi wa Umma kujenga tabia ya kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali yaliyoainishwa katika Benki hiyo na kukata bima ya mali zao ili inapotokea majanga basi bima hiyo iwasaidie kufidia upotevu wa mali zao kulingana na bima waliyokata.