Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

KATIBU MKUU-UTUMISHI AWASISITIZA WATUMISHI WA UMMA KUFANYA KAZI KWA BIDII ILI KULETA TIJA KATIKA JAMII


 

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi, amewasisitiza Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi la Ofisi yake kufanya kazi kwa bidii na weledi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za utendaji ili kuleta mabadiliko yenye tija kwa maendeleo ya taifa.

Bw. Mkomi ameyasema hayo leo tarehe 12 Machi, 2026 wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora uliolenga kupitisha Mpango na Bajeti ya Ofisi hiyo ya Mwaka wa Fedha 2026/27 uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.

“Katika kufikia Utumishi wa Umma uliotukuka, nitoe wito kwa wajumbe wote wa baraza, kutekeleza majukumu yenu ipasavyo ili kutoa huduma bora itakayotatua changamoto za wananchi.” Bw. Mkomi alisema.

Aidha Katibu Mkuu Mkomi amewataka wajumbe wa mkutano huo kuhakikisha kunakuwa na ushirikishwaji wa Watumishi katika mikakati inayopangwa na  kamati hiyo ili kuongeza uelewa wa masuala ya kiutumishi na kuwa na mtazamo chanya utakaoleta ufanisi katika utendaji wao .

Ameongeza kuwa ni muhimu kukawa na mafunzo kwa wajumbe wa Baraza hilo ili kuwajengea uwezo kwa matokeo chanya katika maeneo yao ya kazi.

Bw. Mkomi alimshukuru mwakilishi wa Katibu Mkuu TUGHE Taifa, ambaye ni Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Dodoma Bw. Maulidi Kipeneku kwa ushiriki wake katika mkutano huo na kuahidi kuwa Ofisi ya Rais-UTUMISHI itashirikiana na TUGHE wakati wote katika kuhakikisha Baraza linatekeleza majukumu yake kikamilifu.

Awali Bw. Kipenuke aliipongeza Ofisi hiyo kwa kuzingatia sheria ya kufanya baraza ya wafanyakazi kwa wakati. “Mmekuwa kioo, mabaraza yanafanyika kwa wakati na ni shirikishi, huku akiwatasisitiza wajumbe kutoa michango yao ili kuwawakilisha kwa ufasaha watumishi katika Idara na Vitengo vyao.” Alisisitiza Bw. Kipenuke.