Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

KATIBU MKUU MKOMI: MAFUNZO YATAWAEPUSHA WATUMISHI KUNASWA NA MITEGO YA WAHALIFU MTANDAONI


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais UTUMISHI Bw. Juma Mkomi ametoa rai kwa Watumishi wa ofisi yake kusikiliza, kujifunza na kufuatilia kwa makini njia zinazotumiwa na wahalifu mitandaoni ili kuepuka kunaswa na mitego yao ambayo inaweza kuhatarisha usalama wa utendaji kazi Serikalini.

 Bw. Mkomi ametoa rai hiyo wakati akifungua mafunzo ya uelewa wa usalama wa mitandao na mifumo ya TEHAMA kwa watumishi wa Ofisi yake yanayofanyika katika Ofisi hizo zilizopo Mtumba Jijini Dodoma.

Bw. Mkomi ameongeza kuwa mafunzo hayo yanatokana na changamoto za kimtandao ambazo zinaonekana duniani, hivyo watumishi wa umma nchini Tanzania hawanabudi kujengewa uwezo na uelewa kuhusu masuala ya usalama wa kimtandao ili kuwa tayari kupambana na mbinu za wahalifu wa kimtandao.

“Sisi tunatakiwa kuwa na uelewa mpana wa masuala ya Usalama wa kimtandao kabla ya kwenda kuwafundisha watumishi wengine katika maeneo yao ya kazi” alisisitiza Bw. Mkomi.

Awali, mratibu wa mafunzo hayo ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za TEHAMA Serikalini kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Priscus Kiwango alieleza kuwa katika mafunzo hayo, watumishi watajifunza kuhusu uelewa kuhusu dhana ya usalama wa mifumo na mitandao ya TEHAMA, kulinda vifaa  na mifumo ya TEHAMA, kutambua na kukabiliana na matishio ya usalama wa mitandao, kuwawezesha watumishi juu ya usalama wa mitandao mahala pa kazi na nyenzo za ziada katika usalama wa mitandao kwa watumishi.