Habari
KATIBU MKUU MKOMI AWATAKA WATUMISHI KUONGEZA KASI YA UTENDAJI KUFIKIA MALENGO YA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi, amewataka Watumishi wa Umma kuongeza kasi ya utendaji na kuzingatia weledi ili kuchangia kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Katibu Mkuu Mkomi ametoa wito huo leo Julai 13, 2026, wakati akihitimisha mafunzo kuhusu umuhimu wa afya ya akili kwa Watumishi wa Umma yaliyofanyika katika eneo maalumu la Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Mtumba, jijini Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watumishi hao.
Bw. Mkomi amesema mafanikio ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yanategemea uwepo wa Watumishi wa Umma wenye afya bora ya akili, maadili ya kazi, ubunifu na uwajibikaji, huku akisisitiza kuwa afya ya akili ni msingi wa utendaji wenye tija na utoaji wa huduma bora Serikalini.
"Afya ya akili si suala la mtu mmoja mmoja, bali ni msingi wa kuongeza tija katika Utumishi wa Umma. Mtumishi mwenye afya bora ya akili anakuwa na uwezo mkubwa wa kutoa huduma bora, kushirikiana na wenzake na kuleta matokeo chanya kwa Taasisi na Taifa kwa ujumla," amesema Bw. Mkomi.
Aidha, Bw. Mkomi amewaelekeza Wachumi wa Ofisi hiyo kufanya tafakuri za kitaaluma na kuibua mawazo bunifu yatakayochangia Serikali kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Bingwa wa Afya ya Akili kutoka Jeshi la Polisi Makao Makuu Dodoma, Dkt. Elihuruma Elias, ambaye alikuwa Mwezeshaji wa mafunzo hayo, amesema afya ya akili ni nguzo muhimu ya ustawi wa mtumishi na ina mchango mkubwa katika kuongeza tija pamoja na kuboresha mazingira ya kazi.
Ameeleza kuwa changamoto za afya ya akili kwa watumishi wa Umma mara nyingi husababishwa na mpangilio duni wa kazi, mzigo mkubwa wa majukumu unaozidi uwezo wao, kazi za kujirudia rudia na mazingira magumu ya kazi. Amewahimiza watumishi kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi ya mara kwa mara, kula lishe bora, kupata mapumziko ya kutosha na kutafuta ushauri wa Wataalamu wanapokabiliwa na changamoto za afya ya akili.
Aidha, Dkt. Elias amewataka viongozi kuendelea kuzingatia usawa kwa watumishi wanaowasimamia, kupinga unyanyapaa dhidi ya wenye changamoto za afya ya akili na kutambua mapema dalili za changamoto hizo ili kuwawezesha watumishi kupata huduma stahiki kwa wakati.
