Habari
KATIBU MKUU MKOMI AWASISITIZA WATUMISHI WA UMMA KUFANYA KAZI KWA UPENDO NA USHIRIKIANO
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amewasisitiza watumishi wa umma kote nchini kufanya kazi kwa ushirikiano na upendo ili kufikia malengo ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Katibu Mkuu Mkomi ameyasema hayo leo tarehe 21.11.2024 ofisini kwake katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma akiadhimisha siku ya kuzaliwa kwake.
Amesema watumishi wanatumia muda mwingi sana sehemu za kazi kuliko nyumbani hivyo ni vizuri wakaishi kwa upendo na mshikamano ili kufikia malengo ya serikali ya kuwahudumia wananchi.
Ameongeza kuwa sehemu ya kazi ambayo haina upendo na ushirikiano kunakuwa hakuna amani na matokeo yake watumishi hushindwa kufanya kazi kwa ufasaha.
“Mahali pa kazi ndio sehemu ya kujenga upendo na kuleta amani kwa watumishi wote kwani tusipofanya hivyo tutashindwa kuwahudumia wananchi kikamilifu na kurudisha nyuma maendeleo ya taifa letu.” Bw. Mkomi amesisitiza.
Katibu Mkuu Mkomi ametumia fursa hiyo ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake kwa kuwashukuru Viongozi, Menejimenti na Watumishi wote wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa upendo na ushirikiano ambao wamekuwa wakimpatia katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amempongeza katibu Mkuu Mkomi kwa kuongeza mwaka mwingine katika utumishi wa umma na kuwahamasisha watumishi wa umma wote nchini kufanya kazi kwa umoja jambo ambalo linaleta amani na upendo katika maeneo ya kazi kama ilivyo kwa Ofisi ya Rais-UTUMISHI.
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Musa Magufuli, amempongeza Katibu Mkuu Mkomi kwa kuongeza mwaka mwingine na kuahidi kuendeleza upendo na mshikamano kwa watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI.