Habari
KATIBU MKUU MKOMI AWAASA WATUMISHI WA OFISI YAKE KUJITATHMINI WANAPOTOA HUDUMA KWA UMMA

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amewaasa watumishi wa ofisi hiyo kujitathmini wanapotoa huduma kwa umma wakiwemo Watumishi wa Umma kutoka katika taasisi mbalimbali, Wadau na Wananchi wanaohitaji kuhudumiwa kwenye masuala ya kiutumishi.
Bw. Mkomi ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa ofisi yake katika eneo maalum la mafunzo kwa watumishi hao yanayofanyika kila siku ya Jumatatu Mtumba Jijini Dodoma.
“Ofisi yetu inatoa huduma mbalimbali za kiutumishi, ninawaasa mjitathmini kwa namna mnavyotoa huduma kwa Watumishi wa Umma, Wadau na Wananchi ili tupate mrejesho mzuri kutoka kwao na hatimae kufikia malengo ya Serikali katika kutoa huduma bora kwa kila Mtanzania.” amesema Bw. Mkomi.
Kwa upande wake Mwezeshaji wa mafunzo Balozi Omar Kashera amesema ni vizuri kuwa na uzalendo wa kujenga taswira nzuri ya ofisi kwa kuwa na viongozi bora, kufanya maamuzi sahihi kwa Watumishi wa Umma, Wadau na Wananchi wanaowahudumia ikiwa ni pamoja na kufikiri kwa kina, kushirikisha watumishi wanaofanya nao kazi ili kupata maamuzi jumuishi yatakayokuwa sahihi kwa maslahi ya Taifa.