Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

KATIBU MKUU MKOMI ASISITIZA DHANA YA URITHISHANAJI MADARAKA KWA WATUMISHI WA UMMA NCHINI


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi ameitaka Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu katika Ofisi hiyo kuongeza nguvu katika eneo la mafunzo ya umuhimu wa  Urithishanaji wa madaraka kwa Watumishi wa Umma huku akiwataka Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi nchini kuwaandaa watumishi wao ili waweze kuwa viongozi wazuri hapo baadaye

Amesema Kiongozi mzuri ni yule anayewaandaa watumishi walio chini yake kuwa viongozi wazuri katika siku za usoni huku akionya dhana potofu iliyojengeka kuwa ukiwaandaa watumishi walio chini yako wataichukua nafasi uliyonayo

Amesema Serikali ina Taasisi nyingi ambazo zinahitaji watumishi hao walioandaliwa vizuri na kwa muda mrefu

Bw. Mkomi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Agosti 18, 2025 katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi hiyo  mara baada ya kutolewa kwa mafunzo ya Uongozi,  ikiwa ni muendelezo wa mafunzo hayo ambayo hutolewa  kila wiki kwa Watumishi   kwa  lengo la  kuboresha utendaji kazi wao

Amesema endapo kutakuwa na utamaduni huo wa kurithishana madaraka, watumishi watakaoandaliwa wataenda kuwa viongozi mahali pengine na sio lazima wabaki hapo hapo.  

Awali Mwezeshaji wa Mafunzo hayo ya Uongozi, Dkt. Ntangeki Nshala amesema Uongozi sio lazima uwe unawaongoza watu bali ni kuonesha uwezo ulionao katika eneo ulilopo

Amesema  uongozi ni suala binafsi na msukumo uliopo ndani ya mtu ndio maana uongozi unatofautiana katika ya mtu na mtu

Amesema uongozi ni kuonesha njia,kujaribu  na kujiamini katika kufanya maamuzi popote ulipo na sio lazima uwe na cheo fulani

Aidha Dkt. Nshala amesema Watumishi wanahitaji kuwa na ujasiri  na ndoto kubwa ya kufanya  chochote wanachohitaji   huku akionya tabia ya watu wengi ya kushindwa kuonesha uwezo wao kwa kisingizio cha uroho wa madaraka 

Amesema Watumishi waliowengi mara baada ya kuajiriwa husahau kusudi la ndoto zao na hivyo hujikuta wakiishi ili mradi kwa sababu hali zao za kiuchumi huwa zimeimarika kidogo 

" Ukiwa huna ujasiri huwezi kufanya mambo makubwa na hivyo  wengi hujikuta  wakijidumaza" amesisitiza Dkt. Nshala 

Kufuatia hatua hiyo, Dkt. Nshala amesisitiza watumishi kujitambua na kuwa na dira na maono  ya kutaka kuwa nani katika kazi na kwenye jamii kwa ujumla