Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

KATIBU MKUU MKOMI AONGOZA KIKAO CHA KAMATI KUU YA UFUATILIAJI NA TATHIMINI


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Mkomi ameongoza Kikao cha Kamati Kuu ya Ufuatiliaji na Tathmini kilichojadili Taarifa ya Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Rais – Utumishi kwa Robo ya Nne ya Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Kikao hicho kimefanyika leo Septemba 01, 2026 katika ukumbi wa Nyaraka Jijini Dodoma kwa lengo la kupitia na kutathmini kiwango cha utekelezaji wa majukumu, mipango, shughuli na malengo yaliyowekwa na Ofisi katika kipindi cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Bw. Mkomi amesisitiza umuhimu wa ufuatiliaji na tathmini katika kuhakikisha kuwa mipango na shughuli za Ofisi zinatekelezwa kwa ufanisi, kwa wakati na kwa kuzingatia viashiria vya utendaji vilivyowekwa.

Amesema ufuatiliaji na tathmini ni nyenzo muhimu katika kupima matokeo ya utekelezaji wa mipango ya Serikali, kutambua maeneo yanayohitaji maboresho na kuwezesha uongozi kufanya maamuzi yanayozingatia ushahidi.

“Ni muhimu taarifa za ufuatiliaji na tathmini zisitumike tu kwa ajili ya kuonesha kiwango cha utekelezaji, bali pia ziwe msingi wa kufanya maboresho na kuchukua hatua stahiki pale ambapo utekelezaji haujafikia malengo yaliyokusudiwa,” amesema Bw. Mkomi.

Katika hatua nyingine, amewataka viongozi na watendaji wa Ofisi kuhakikisha utekelezaji wa majukumu yao unaendana na mipango na vipaumbele vilivyowekwa, huku wakizingatia matumizi bora ya rasilimali, uwajibikaji na utoaji wa huduma zenye tija kwa wananchi.

Pamoja na mambo mengine, kamati pia imejadili maeneo yanayohitaji kuimarishwa katika kipindi kijacho, ikiwemo kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mipango, kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa shughuli na kuhakikisha taarifa za utendaji zinawasilishwa kwa wakati na kwa kuzingatia viashiria vilivyowekwa.