Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI Eng. ZENA AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KUHESHIMIANA


Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Mhandisi Zena Ahmed Said amesisitiza Mameneja Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Barani Afrika, Tawi la Tanzania kuwaheshimu watumishi wote wa umma hata kama ni wa kada ya chini kwa kuwa kila mmoja anamchango wake kwa ustawi wa taasisi na Taifa kwa jumla.

Mhandisi Zena ametoa kauli hiyo leo Mei 6, 2024 wakati wa kufungua Mkutano wa Mameneja Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Barani Afrika, Tawi la Tanzania unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

“Tunahitaji kutoa heshima kwa kila mtu kwa kuwa kila binadamu anastahili heshma, iwapo tutawadharau wahudumu wetu kwa kuona kuwa ni kada ya chini tutajikuta tutakosa watu wa kutuhudumia, hivyo tutashindwa kufanya kazi zetu za msingi”ameongeza Mhandisi Zena.

Aidha, Mhandisi Zena amewakumbusha Mameneja hao kutambua kuwa, vyeo vya watumishi wa umma kwa kada zote ni muhimu sana na viliwekwa kwa sababu maalum. Kwa mantiki hiyo, kila mtumishi kwa nafasi yake anatakiwa kuheshimiwa kwa kuwa anamchango katika kuhakikisha dira ya taifa inafikiwa kwa haraka na kwa ufanisi.

Vilevile, amewataka Mameneja hao kuwa wazalendo, kutamani kuona maendeleo ya Taifa, kutotaja majina ya viongozi wakuu bila sababu ya msingi kuwa wamepewa maelekezo kutoka juu, kuacha tabia ya kubeza kwa namna yoyote ile siku na sherehe za kitaifa, isipokuwa wanatakiwa kuziheshimu na kuzienzi kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Awali, Rais wa Mtandao wa Mameneja Rasilimaliwatu Barani Afrika ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi, amesema kuwa mtandao huo unatumika kama njia ya kuweka pamoja Mameneja Rasilimaliwatu Barani Afrika na kubadilishana uzoefu wa namna ya kuboresha utendaji kazi katika nchi zao kwa lengo la kuleta maendeleo ya haraka.

“Sasa hivi tunashuhudia matumizi makubwa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano -TEHAMA katika utendaji kazi, hivyo uwepo na ukuaji huu wa teknolojia mathalani matumizi ya Akili Bandia (Artificial Intelligence-AI) hatuna budi kama Bara la Afrika kuongeza jitihada za ukuaji wa Mtandao huu ili nchi zote Barani Afrika ziweze kutumia teknolojia hizi kwa maendeleo” amebainisha Bw. Daudi.

Aidha, ameongeza kuwa Mtandao utasaidia Bara la Afrika kuwa na wataalamu wa rasilimaliwatu wenye sifa na ubora ili waweze kuzisaidia nchi zao kujikwamua kiuchumi na kuleta maendeleo.

Pia, Bw. Daudi ametumia fursa ya mkutano huo kuhamasisha watu kushiriki kwa wingi kwenye mkutano wa mwaka wa Bara la Afrika ambao utafanyika mwezi Novemba, 2024 nchini Tanzania. Mkutano huo utatumika kubadilisha uzoefu na zaidi kukuza na kuongeza uchumi wa Taifa.

Mkutano huo ulifanyika kwa siku moja umetumika kuzindua rasmi Mtandao wa Mameneja Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Barani Afrika, Tawi la Tanzania (TPS-HRMnet).