Habari
KATIBU MKUU KIONGOZI DKT. KUSILUKA AELEKEZA TAASISI ZA UMMA KUWA NA PROGRAMU MAALUM YA MICHEZO

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka amezielekeza Ofisi za Umma kuwa na programu maalum ya michezo kwa Watumishi wa Umma ili kuimarisha afya zao na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa ustawi wa taifa.
Balozi Dkt. Kusiluka amezungumza hayo leo tarehe 10 Agosti, 2024 katika Bonanza la Michezo ya SHIMIWI lililofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ikiwa ni maandalizi ya michezo ya SHIMIWI inayotarajia kuanza tarehe 18 Septemba hadi 05 Oktoba, 2024 mkoani Morogoro.
Balozi Dkt. Kusiluka ametoa rai kwa Wizara na taasisi zote za umma kutenga bajeti na muda kwa ajili ya michezo kwa watumishi wa umma ili waweze kushiriki kwa lengo la kuimarisha afya zao, kudumisha umoja na ushirikiano.
Aidha, Dkt. Kusiluka amempongeza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa kwa kushiriki katika maandalizi ya bonanza hilo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi amesema kuwa agizo la Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka la kutaka Ofisi za Umma kuwa na programu maalum ya michezo kwa watumishi wa umma ni jambo jema kwani itawahamasisha zaidi kutunza afya zao na kuwawezesha kutekeleza majukumu na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Vilevile, Bw. Mkomi ameongeza kuwa ofisi yake imekuwa ikishiriki kliniki za afya kwa watumishi wa umma ambapo hivi karibuni ilishirikiana na Hospitali ya Benjamin Mkapa katika kambi maalum ya zoezi la upimaji afya wa hiari katika maeneo ya ofisi za Serikali Mtumba lengo likiwa kuimarisha afya za watumishi wa umma.
Viongozi na Watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI, wameshiriki katika bonanza hilo ambalo hufanyika kila mwaka, na Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Michezo Huboresha Utendaji kazi, Shiriki Uchaguzi wa serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu.”