Habari
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YAPOKEA TAARIFA YA UTENDAJI WA TUME YA UTUMISHI WA UMMA, YASISITIZA UTOAJI WA ELIMU KUHUSU RUFAA NA MALALAMIKO KWA WATUMISHI WA UMMA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imepokea taarifa ya utendaji wa Tume ya Utumishi wa Umma na kusisitiza kutolewa kwa elimu zaidi kwa Watumishi wa Umma ili waweze kuwasilisha rufaa na malalamiko kwa wakati na mahali husika kwa lengo la kutimiza haki na wajibu katika utendajikazi.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro alipokuwa akiongoza kikao cha Kamati yake na Watendaji wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Tume ya Utumishi wa Umma kilicholenga kupokea taarifa ya Utendaji wa Tume hiyo katika kushughulikia rufaa na malalamiko kutoka kwa Watumishi wa Umma na Mamlaka za Ajira.
“Elimu inahitajika zaidi kwa Watumishi wa Umma kwenye maeneo yao ya kazi ili kuongeza uelewa wa namna ya kushughulikia rufaa na malalamiko hayo ikiwa ni pamoja na kupata utatuzi wa migogoro katika Utumishi wa Umma,’’ Amesisitiza Mhe. Dkt. Ndumbaro
Katika hatua nyingine, Mhe. Dkt. Ndumbaro amempongeza na kumshukuru Waziri Kikwete kwa taarifa nzuri aliyoiwasilisha kwa Kamati hiyo iliyoelezea kwa kina taarifa ya utendaji ya Tume ya Utumishi wa Umma katika kushughulikia rufaa na malalamiko kutoka kwa Watumishi wa Umma na Mamlaka za Ajira ambayo itaongeza chachu ya utendaji kazi kwa Watumishi wa Umma.
Mhe. Dkt. Ndumbaro ameiahidi Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora kuwa itashirikiana nayo katika usimamizi wa masuala mbalimbali ili kuleta matokeo chanya kwa ustawi wa Taifa.
Awali akiwasilisha kwa Kamati hiyo taarifa ya utendaji ya Tume ya Utumishi wa Umma katika kushughulikia rufaa na malalamiko kutoka kwa Watumishi wa Umma na Mamlaka za Ajira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema, Tume ya Utumishi wa Umma ni Mamlaka ya Rufaa kwa Watumishi wa Umma katika taasisi 554 waliopo kwenye makundi mbalimbali ya Watumishi wa Umma, Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Watumishi waliopo katika Taasisi za Umma.
Vilevile, Mhe. Kikwete amesema Tume hiyo ina jukumu la kupokea malalamiko na rufaa kutoka kwa Watumishi wa Umma ambao hawakuridhika na uamuzi wa mamlaka zao za ajira, mamlaka za nidhamu na waajiri baada ya uamuzi walioufanya na mamlaka hizo hivyo, elimu itakayotolewa kwa Watumishi wa Umma itasaidia kwa kiasi kikubwa kupata haki na wajibu kwa kila mmoja.
Aidha, Mhe. Kikwete ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kwa kuwa na majadiliano mazuri na ofisi anayoiongoza ambayo wanaamini yatawasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza ufanisi na utendaji wa majukumu yao.
“Mhe. Mwenyekiti, nitoe shukrani za dhati kwa niaba ya ofisi ninayoiongoza mara zote tumepokea maoni, ushauri na michango mbalimbali kutoka katika Kamati yako inayolenga kuboresha Utumishi wa Umma nchini kwa lengo la kutimiza azma ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na Utumishi wa Umma uliotukuka.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi amesema Kamati hiyo imekuwa msaada mkubwa wa kuiongoza Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora kwa kuwapatia maarifa mengi kutoka kwa Wajumbe wote wa Kamati hiyo yenye kuleta tija katika kuwahudumia wadau mbalimbali na kuboresha utendajikazi.
