Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA KATIBA NA SHERIA YAIPONGEZA OFISI YA RAIS-UTUMISHI NA TAASISI ZAKE KWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE KIKAMILIFU


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeipongeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na taasisi zake kwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kuishirikisha Kamati hiyo na kutoa uelewa mpana kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na ofisi hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama ametoa pongezi hizo leo jijini Dodoma kwa niaba ya kamati yake wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo na Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kiliyolenga kupokea na kujadili taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2025/26.

“Kamati inatoa pongezi nyingi kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na taasisi zake kwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu jambo linalodhihirisha kuwa mnaendana na maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na Serikali inayotekeleza majukumu yake kikamilifu kwa maendeleo ya nchi.” Mhe. Mhagama amesema.

Mhe Mhagama ameitaka Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora pamoja na taasisi zake kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ili kuleta tija na manufaa nchini yatakayokidhi mahitaji na viwango vikubwa katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kwa kutoa ushauri, maoni na miongozo mbalimbali ambayo ofisi yake imekuwa ikiifanyia kazi na kwa asilimia kubwa imeisaidia ofisi hiyo kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

“Mhe. Mwenyekiti, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora inajivunia kusimamiwa na Kamati yako kwani mmekuwa mkitupatia ushauri, maoni na miongozo mbalimbali ambayo yameleta tija kwetu na kutufanya tutekeleze majukumu yetu kikamilifu na kwa ufanisi mkubwa sana.” Mhe. Simbachawene amesema.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria itapokea taarifa ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na taasisi zake kwa siku mbili tarehe 26 na 27 Machi, 2025 kwa lengo la kujadili Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2025/26.