Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI (PAC) YAIPONGEZA eGA KWA KULETA MABADILIKO KATIKA UTUMISHI WA UMMA


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhe. Japhet Hasunga na wajumbe wa kamati yake wameipongeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia taasisi yake ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kuleta mabadiliko katika utumishi wa umma kupitia Mifumo ya TEHAMA ambayo imerahisisha upatikanaji wa huduma bora nchini.

Mhe. Hasunga ameyasema hayo leo wakati kamati yake ilipofanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) ambacho kipo chini ya Mamlaka ya Serikali Mtandao.

“Kamati yetu imefurahishwa sana na utendaji kazi wa wataalam wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na taasisi yake ya Mamlaka ya Serikali Mtandao eGA kwani haya yote tunayoyaona ni sehemu ya mabadiliko ya kuboresha utumishi wa umma nchini, kipindi cha nyuma haikuwa rahisi watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kupitia Mifumo ya TEHAMA,” Mhe. Hasunga amesema. 

Mhe. Hasunga ameipongeza eGA kwa jitihada kubwa inazofanya za kuunganisha mifumo ya TEHAMA iliyopo kwenye taasisi za umma ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi kwa wakati na mahali popote.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Kituo kinafanya utafiti na kubuni mifumo ya TEHAMA Serikalini yenye uwezo kuongeza kasi katika jitihada za utoaji wa huduma kwa umma kwa haraka na gharama nafuu.

Mhe. Kikwete ameishukuru Kamati kwa kupanga ziara hiyo muhimu katika  kituo  ambapo ushauri na maelekezo yamepokelewa na Ofisi yake iko tayari kusimamia utekelezaji wake ili wananchi waweze kunufaika na uwepo wa teknolojia.

Naye, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amewahakikishia wajumbe wa kamati hiyo kuwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itaendelea kuisimamia Mamlaka ya Serikali Mtandao ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kuziwezesha taasisi za umma kutumia TEHAMA kwa lengo la kuboresha utoaji huduma kwa umma.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Eng. Benedict Ndomba ameishukuru kamati hiyo kwa kufanya ziara ya kikazi katika kituo hicho na kuahidi kuendelea kubuni mifumo mbalimbali kwa maendeleo ya taifa.