Habari
KAMATI YA KITAIFA YA KUDHIBITI VVU, UKIMWI NA MSY MAHALI PA KAZI KATIKA UTUMISHI WA UMMA YATAKIWA KUIMARISHA MALENGO YA KUDHIBITI MAGONJWA HAYO

Kamati ya kitaifa ya kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza (MSY) mahali pa kazi katika Utumishi wa Umma ambayo inajumuisha Waratibu ngazi ya halmashauri, mkoa na kitaifa, imetakiwa kuimarisha malengo ya kudhibiti magonjwa hayo kwa kuhakikisha Wizara, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinasimamia utekelezaji wa Mwongozo wa kudhibiti VVU, UKIMWI na MSY na uwasilishwaji wa taarifa kwa wakati .
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Musa Magufuli kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI katika ufunguzi wa kikao kazi cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa Afua za VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025 ngazi ya Mkoa na Taifa.
Bw. Magufuli amesema, ili kufikia malengo ya kudhibiti magonjwa hayo, mafunzo ya kuwajengea watumishi uwezo wa namna ya kudhibiti yanatakiwa kutolewa na kuteua Kamati za Kudhibiti VVU, UKIMWI na MSY katika utumishi wa Umma.
Aidha, Bw. Magufuli, amesema kwa kutambua umuhimu wa Afya na Ustawi wa Watumishi wa Umma nchini, Ofisi ya Rais-UTUMISHI iko katika hatua za mwisho za kukamilisha Mwongozo na Waraka kuhusu kudhibiti VVU, UKIMWI na MSY ikiwemo na changamoto za Afya ya Akili mahali pa kazi katika Utumishi wa Umma.
Bw. Magufuli amewashukuru na kuwapongeza wakuu wa Taasisi za umma nchini kwa kutekeleza kikamilifu afua za kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukizwa na kusisitiza kuwa Ofisi ya Rais-UTUMISHI itaendelea kufanya ufuatiliaji kwa lengo la kubaini mafanikio na changamoto za utekelezaji.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Bw. Balandya Elikana, ametoa rai kwa kila halmashauri kendelea kutekeleza Mwongozo wa VVU, UKIMWI na Magonja Sugu Yasiyoambukiza (MSY) mahali pa kazi katika Utumishi wa Umma kwa masilahi mapana ya taifa.