Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

KAMATI YA BUNGE YAPITISHA MAKADIRIO YA BAJETI YA MWAKA 2024/25 YA TAASISI ZILIZO CHINI YA OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA


 

Na Lusungu Helela-Dodoma


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imepitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 ya Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. 

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Florent Laurent Kyombo akikaimu nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo leo Machi 23, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Bunge Jijini Dodoma mara baada ya wajumbe wa Kamati kujadili na kuridhia bajeti katika kikao kilichohusisha Kamati hiyo na Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.  

Amesema baada ya majadiliano mazuri na maelezo ya ziada kutolewa kuhusiana na bajeti iliyotengwa, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria imeridhia. 

“Tunawatakia matumizi mema ya fedha hizi pale zitakapokubaliwa kupitishwa katika vikao vya Bunge la Bajeti na tunahitaji kuona bajeti ya fedha hizi inaakisi matarajio ya msingi ya nchi yetu,” amebainisha Mhe. Kyombo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameishukuru Kamati hiyo kwa ushauri na kupitia bajeti hiyo kifungu kwa kifungu na kutoa maelekezo ya kuboresha kabla ya kuiwasilisha kwenye vikao vya Bunge la Bajeti.

“Mimi pamoja na timu yangu, tunatoa shukrani za dhati kwa jinsi mnavyotoa michango yenu yenye muelekeo wa kuboresha Utumishi wa Umma nchini ili kukidhi matakwa  na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan” amesema Mhe. Simbachawene.