Habari
KAIMU KATIBU MKUU UTUMISHI AVUTIWA NA UBUNIFU WA UTOAJI MAFUNZO KWA WATUMISHI
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amesema amevutiwa na ubunifu wa kipekee unaoendelea kufanywa na Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kwa kuja na mkakati wa kutoa mafunzo elekezi ya pamoja kwa Watumishi wote wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhusu matumizi sahihi ya mfumo wa ofisi mtandao (e-Office)
Bw. Daudi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu tarehe 28 Oktoba, 2024 wakati akizungumza na Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo amesema ujio wa mafunzo ya kujengeana uwezo ni muhimu ikizingatiwa kwa sasa matumizi ya mfumo wa Ofisi Mtandao katika Ofisi za Serikali ni jambo lisiloepukika
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bi. Nyasinde Mukono amesema mafunzo hayo yatakuwa yakifanyika kila Jumatatu asubuhi lengo likiwa ni kuwajengea uwezo watumishi wote.
"Tumekuja na utaratibu huu wa kujumuika kwa pamoja ili kuhakikisha watumishi wote wanakuwa na uelewa wa pamoja wa matumizi sahihi ya mfumo wa ofisi mtandao,” amesema Bi. Mukono.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na Watumishi pamoja na Wakurugenzi wa ofisi hiyo ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo matumizi ya saini ya kidigitali, tahadhari za kiusalama katika matumizi ya mfumo wa ofisi mtandao pamoja na namna bora ya kushughulikia barua kwa njia ya mfumo wa ofisi mtandao.
Mada hizo zilizowasilishwa ziliongozwa na Wataalamu wa kutoka ndani na nje ya Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora zikiongozwa na mwenyeji wao Afisa Tehama Mkuu, Bi. Zalika Hussein.