Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

eGA YAPONGEZWA NA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA KWA KUSANIFU NA KUSIMAMIA MIFUMO YA TEHAMA NCHINI


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeipongeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia taasisi iliyopo chini yake ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kusanifu na kusimamia mifumo mingi ya TEHAMA nchini ili kuboresha utoaji huduma kwa taasisi za umma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama ametoa pongezi hizo leo jijini Dodoma kwa niaba ya kamati yake wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo na Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) na Taasisi ya UONGOZI iliyolenga kupokea na kujadili taarifa ya utendaji kazi wa tassisi hizo.

Mhe Mhagama amesema ni wazi kuwa kwa sasa taasisi zote za serikali zinatumia mifumo ya TEHAMA hivyo, eGA ina wajibu wa kuzisaidia taasisi hizo ili kutimiza malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na serikali ya kidijitali itakayokidhi mahitaji na viwango vikubwa katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

 “Tunafahamu kuwa kila taasisi ya serikali inatumia mifumo ya TEHAMA, niwasihi endeleeni kushirikiana ili kuleta tija na manufaa katika utendaji kazi kwa lengo la kutimiza malengo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na serikali ya kidijitali kwa maendeleo ya nchi yetu.” Dkt. Mhagama amesisitiza

Akizungumzia maeneo ambayo jiografia yake haipo vizuri, Mhe. Dkt. Mhagama amesema maeneo hayo yanapaswa kuwa na miundombinu ya TEHAMA itakayowezesha upatikanaji wa huduma za kimtandao uliosanifiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ili kuwasaidia watumishi wa umma kuendelea kutekeleza majukumu yao bila kuwa na changamoto ya kimtandao.

Katika hatua nyingine, Mhe. Dkt. Mhagama ameipongeza Taasisi ya UONGOZI kwa kuendesha mafunzo ya mara kwa mara kwa viongozi jambo ambalo linawasaidia watumishi katika taasisi mbalimbali kuwajibika kwa ufasaha kupitia mafunzo ambayo wamekuwa wakipatiwa kutoka katika taasisi hiyo.

Ameisisitiza taasisi hiyo kuendelea kuwajengea uwezo viongozi waliopo ili kuwa na viongozi bora na wazalendo kwa nchi yetu.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kwa kutoa ushauri, maoni na miongozo mbalimbali ambayo ofisi yake imekuwa ikiifanyia kazi na kwa asilimia kubwa imeisaidia ofisi hiyo kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

“Mhe. Mwenyekiti, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora inajivunia kusimamiwa na Kamati yako kwani mmekuwa mkitupatia ushauri, maoni na miongozo mbalimbali ambayo yameleta tija kwetu na kutufanya tutekeleze majukumu yetu kikamilifu na kwa ufanisi mkubwa sana.” Mhe. Simbachawene amesema.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imemaliza kikao kazi chake cha siku mbili kwa kupokea na kujadili taarifa ya utendaji kazi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na baadhi ya taasisi zake ikiwemo TASAF, eGA na Taasisi ya UONGOZI.