Habari
DKT. KANUWA; UTUMISHI WA UMMA NI KAZI YA MUNGU
“Tambueni kuwa Utumishi wa Umma ni kazi ya Mungu, fanyeni uamuzi kwa kuzingatia sheria za nchi na za kimataifa na msiwe na jaziba, visasi wala upendeleo ili kulinda maslahi ya Taifa”
Wito huo umetolewa Novemba18, 2024 na Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Taaluma Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, Dkt. Juma Kanuwa wakati akifanya wasilisho kuhusu Maslahi ya Taifa kwa Watumishi wa Ofisi ya Rais, UTUMISHI Mtumba, Jijini Dodoma.
Ameongeza kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ni muhimu kwa ustawi wa Taifa la Tanzania kwa kuwa inasimamia rasilimaliwatu, hivyo, Watumishi wake wanatakiwa kufanya uamuzi wakati wote kwa kuzingatia uadilifu, falisafa ya nchi, uwezo wa nchi kiuchumi, rasilimali zilizopo na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Amewasisitiza pia Watumishi kupendekeza jambo la maendeleo kwa kuzingatia miongozo na kufuata ngazi za madaraka, uzalendo na hatimaye viongozi waweze kufanya uamuzi kwa kwa kuzingatia ilani ya chama husika na Maslahi mpana ya taifa.
“Ni fahari kubwa kuitumikia nchi yako kwa umahiri na uwezo mkubwa na epuka kuwa na kinyongo unapotekeleza majukumu ya Kitaifa kwa kuwa maslahi ya taifa yanaanzia kwa mtu binafsi” Dkt. Kanuwa.
Akihitimisha mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi hao, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala Bw. Musa Magufuli alimshukuru Dkt. Kanuwa kwa kutoa elimu hiyo kwa watumishi wake na ameahidi kuchukua wasilisho hilo na kulisambaza kwa watumishi wote ili waendelee kujifunza ingawa haitaondoa dhana ya kuita wawezeshaji kutoa elimu hiyo.
Mafunzo hayo ni mwendelezo wa utaratibu uliowekwa na Ofisi hiyo wa kutoa uelewa kuhusu masuala mbalimbali katika Utumishi wa Umma ili kutekeleza majukumu yao ipasavyo.