Habari
DAFTARI LA HUDUMA ZA SERIKALI (GSD) KUIMARISHA UTOAJI WA HUDUMA ZA UMMA KWA NJIA YA KIDIJITI
Daftari la Huduma za Serikali (GSD) ni Mfumo wa kidijitali ambao unalenga kuwapatia wananchi, wafanyabiashara na wageni fursa taarifa na maombi ya huduma za serikali katika Wizara, Idara, Wakala, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa hivyo, kurahisisha utoaji wa huduma kwa umma kwa njia ya kidijiti.
Hayo yameelezwa leo na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Mifumo na Viwango vya Kimenejimenti kutoka Idara ya Uendelezaji Taasisi, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Noah Mkasanga wakati akiwasilisha mada kuhusu Daftari la Huduma za Serikali kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo Watumishi wa Ofisi hiyo iliyopo Mtumba Jijini Dodoma.
Bw. Noah amesema kuwa, kupitia mfumo wa GSD wananchi wataweza kupata huduma zote za Serikali kidijitali kupitia dirisha moja, ikiwa ni pamoja na kuona huduma zinazotolewa, gharama zake, masharti au vitu vinavyohitajika ili kupata huduma na namna ya kuzipokea hata wakiwa nyumbani kwa kutumia anwani za makazi (NAPA).
“Daftari hili linarahisisha utoaji wa huduma mbalimbali za Serikali kwa umma kupitia dirisha moja kwa kuainisha huduma zote zinazotolewa na taasisi za umma pamoja na mahitaji yao na kuziweka wazi kwa wananchi wanapotaka kupata huduma husika kwa njia ya kidijiti”, amesema Bw. Noah.
Akifafanua kuhusu umuhimu wa Daftari la Huduma za Serikali (GSD) Bw. Noah amesema, litaongeza ufanisi na uwajibikaji ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama kwa wateja na urahisi wa kutoa huduma kupitia mfumo mmoja.
Kadhalika, Bw. Noah, amesema kuwa Daftari la Huduma za Serikali (GSD) litasaidia kupunguza mianya ya rushwa kwa kuwa huduma hiyo inatolewa kwa njia ya kidijitali.
Kuanzishwa kwa Daftari la Huduma za Serikali (GSD) ni jitihada za Serikali za kutumia teknolojia ya kisasa katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuimarisha usalama wa taarifa za umma.
