Habari
CHANGAMOTO ZA WATUMISHI WA UMMA ZITATULIWE ILI KUKUZA SEKTA YA UMMA KIUCHUMI NA KIJAMII
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewaasa Mameneja Rasilimaliwatu katika Sekta ya Umma Afrika (APS-HRMNet) kuwa wabunifu katika kusimamia vizuri rasilimaliwatu ili kuondokana na changamoto mbalimbali za watumishi wa umma na kukuza sekta hiyo kiuchumi na kijamii ili kuleta maendeleo makubwa katika Bara la Afrika.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo alipokuwa akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa kufungua Mkutano wa 9 wa Mtandao wa Mameneja wa Rasilimaliwatu katika Sekta ya Umma Afrika (APS-HRMNet) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
“Mkutano huu wa Mtandao wa Mameneja Rasilimaliwatu umefanyika katika kipindi ambacho dunia ina changamoto mbalimbali hivyo niwaase mtumie fursa ya mijadala mtakayoiendesha na mawazo mtakayoyatoa kupitia maazimio na mapendekezo yalete mtazamo chanya katika kutoa majawabu yatakayosaidia kukuza sekta ya umma kiuchumi na kijamii.” Amesema Mhe. Simbachawene
Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa, kupitia kaulimbiu ya mkutano huo inaonyesha ni kwa namna gani rasilimaliwatu katika utumishi wa umma ni nyenzo muhimu na ya thamani kubwa katika kila nchi ambapo Serikali huitumia kuwafikia wananchi wake katika kutoa huduma za kijamii na kiuchumi ili kukuza ustawi wa jamii husika.
Aidha, Mhe. Simbachawene amewapongeza wawezeshaji wa Mkutano huo kwa mada mbalimbali walizozitoa kabla ya kufunguliwa kwa mkutano huo ambazo kwa asilimia kubwa zitasaidia kuleta mabadiliko katika utendaji kazi kupitia rasilimaliwatu zilizopo katika Bara la Afrika.
Kwa upande wake, Rais wa Mtandao wa Mameneja Rasilimaliwatu katika Sekta ya Umma Afrika (APS-HRMNet) ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi, amesema kuwa katika mkutano huo wa 9 wajumbe watapata fursa ya kubadilishana uzoefu na utaalamu kwa lengo la kuwezesha nchi za Bara la Afrika kupiga hatua za kimaendeleo kwa kutumia mbinu za kisasa.
“Mtandao huu umeanzishwa kwa lengo la kujenga uwezo wa rasilimaliwatu yenye matokeo chanya katika kuhudumia wananchi Barani Afrika hivyo kupitia Mkutano huu tutapata fursa ya kubadilishana uzoefu na utaalamu ili kuzisaidia nchi zetu kujikwamua kiuchumi na kuleta maendeleo kwa mataifa.” Bw. Daudi amesema.
Mkutano huo wa Mtandao wa Mameneja Rasilimaliwatu katika Sekta ya Umma Afrika (APS-HRMNet) uliofunguliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan unatarajiwa kufanyika kwa muda wa siku nne kuanzia leo tarehe 4 hadi 7 Novemba, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) jijini Arusha.
Kaulimbiu ya Mkutano huo ni ‘Utawala Stahimilivu na Ubunifu: Kukuza Sekta ya Umma ijayo kupitia Uongozi wa Rasilimaliwatu’.