Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

AJIRA ZA TASAF ZILENGE KUWAKOMBOA WANANCHI KATIKA UMASKINI- Mhe. Simbachawene


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameeleza kuwa dhamira ya Serikali kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika ajira za muda sio kutengeneza barabara kwa mikono bali ni kuwawekea mazingira ya kuwa na ajira itakayowawezesha kupata kipato na kuweza kujitegemea katika kufanya kazi na kujikomboa na wimbi la umaskini.

Mhe. Simbachawene amesema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga.

Amesema wananchi wamekuwa wakifanya kazi za miradi mbalimbali ya TASAF ikiwemo ujenzi wa miundombinu katika maeneo yao akitolea mfano ujenzi wa barabara na kulipwa ujira ili waweze kujikomboa na wimbi la umasikini.

Mhe. Simbachawene ameainisha wanufaika wanaolengwa katika ajira za muda za TASAF kuwa ni wale ambao wanakidhi masharti ya umri ambao si chini ya miaka 18 na si zaidi ya miaka 65. Vilevile asiwe mgonjwa na asilazimishwe kufanya kazi kinyume na vigezo hivyo.

Aidha, amewasisitiza Viongozi wa Serikali kusimamia masharti hayo ili kuepuka wasioweza kufanya kazi hizo kulingana na vigezo vilivyowekwa wasifanye kwa kuwa hiyo sio njia pekee ambayo walengwa wanatakiwa kuwezeshwa na TASAF lakini amewataka vijana wenye uwezo katika kaya kutumia fursa hiyo ya ajira kwa lengo la kuzikomboa kaya zao katika wimbi la umaskini.

Mkinga ni miongoni mwa Wilaya za mfano kwa utekelezaji na usimamizi mzuri wa miradi ya TASAF, ninaona na nimeridhishwa na maonesho ya shughuli zinazofanywa na akina mama ili kujikomboa na umaskini na hatua kubwa iliyopigwa katika utelekezaji wa shughuli zenye lengo la kuondoa umasikini na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii,” alisema.

Mhe. Simbachawene ametumia fursa ya mkutano huo kuwaomba wananchi kufanya dua na sala kumuombea hekima, kheri na baraka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kuwa na moyo wa upendo kwa kuwa ndiye anayetafuta fedha kutoka nje na ndani ya nchi kwa lengo la kuwakomboa wananchi wake kutoka katika wimbi la umasikini.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya TASAF, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mhe. Kanali Maulid Surumbu amesema TASAF kupitia wananchi imetengeneza na kujenga barabara, shule na zahanati ambazo zinawasaidia kwa namna moja ama nyingine kujikomboa na wimbi la umasikini katika wilaya ya yao.

Ameongeza kuwa, wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga katika vijiji vyote wananufaika vyema na uwepo wa TASAF kwa kiwango kikubwa kwa kuwa kaya masikini zimefikiwa na zinawezeshwa kujikwamua kiuchumi.