Habari
AFYA NI MTAJI – KATIBU MKUU MKOMI AWASISITIZA WATUMISHI WA UMMA KUJILINDA
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bw. Juma Mkomi amewasisitiza watumishi wa umma kulinda na kuimarisha afya zao wakati wote ili zitumike kuwajibika ipasavyo na kuwa mtaji katika kuleta matokeo chanya Serikalini.
Bw. Mkomi ameyasema hayo leo Mei 4, 2026 katika eneo maalumu la Ofisi hiyo, Mtumba Jijini Dodoma wakati akihitimisha mafunzo kuhusu fursa za mimea tiba katika kutibu magonjwa mbalimbali.
“Ni vizuri kila mtumishi wa umma akawa na uelewa kuhusu faida za utunzaji wa afya aliyo nayo na kuchukua hatua mapema pindi anapopata changamoto ili kuitumia afya hiyo kuwa mtaji Serikalini na kuleta tija katika maslahi ya umma”. Bw. Mkomi alisema.
Amesisitiza kuwa changamoto ya watumishi wengi kuugua mara kwa mara inapunguza kasi ya utendaji, lakini watumishi wanapokuwa na afya bora, hupunguza kuomba likizo za ugonjwa, na hivyo kuongeza bidii ya kazi.
Aidha, Bw. Mkomi amemshukuru Prof. Joseph Ndunguru ambaye ni Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania, (TPHPA) kwa wasilisho lake ambalo limetoa uelewa kwa watumishi utakaojenga hamasa na kuwa nyenzo muhimu ya kuongeza ufanisi katika kazi.
Awali akiwasilisha mada kuhusu fursa za Mimea Tiba katika Kutibu Magonjwa mbalimbali, Prof. Ndunguru alisema Tanzania ina utajiri mkubwa wa mimea yenye uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali lakini bado inahitaji utafiti wa kisayansi ili kuthibitisha usalama na ufanisi wake.
Aliongeza kuwa matumizi ya tiba asili yaliyofanyiwa tafiti za kisayansi yanapunguza magonjwa, hivyo kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu na kuboresha afya ya watumishi.
Prof. Ndunguru ametoa wito kwa Serikali na Taasisi za Umma kuwekeza katika tafiti ili kuendeleza tiba asili na kuchangia maendeleo ya afya na uchumi wa Taifa.
