Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WITO WATOLEWA KWA WATUMISHI WA OFISI YA RAIS-UTUMISHI KUIISHI MIONGOZO INAYOTOLEWA NA OFISI HIYO


Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Taasisi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Nolasco Kipanda ametoa rai kwa Watumishi wa Ofisi hiyo kuiishi Miongozo ya kiutendaji wanayoitoa kwa Watumishi wa Umma ili kuwa mfano bora wa kuigwa katika utekelezaji wa Miongozo hiyo hasa katika kuwahudumia wananchi.

Mkurugenzi Kipanda ameyasema hayo leo Desemba 8, 2025 alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu-UTUMISHI wakati akihitimisha Mafunzo ya Utoaji Huduma kwa Mteja yaliyotolewa na Chuo cha Serikali za Mitaa-Hombolo kwa watumishi wa Ofisi hiyo Mtumba Jijini Dodoma.

“Asili ya Ofisi yetu ni kutoa huduma, lakini pia sisi ndio tunaotoa miongozo inayoendesha Utumishi wa Umma nchini, hivyo tunapaswa kuiishi kikamilifu na kujenga taswira nzuri ya Ofisi na kuwa mfano kwa maslahi ya taifa,” Bw. Kipanda amesisitiza.

Aidha, amewapongeza watoa mada ya Huduma kwa Mteja kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa-Hombolo kwa mawasilisho yao muhimu ya namna bora ya kuhudumia mteja kwa haraka na kwa wakati.

Kwa upande wake, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo Bi. Scholastica Tibitha alisema kuwa Watumishi wa Umma kwa dhamana waliyonayo wanatakiwa kutambua saikolojia ya mteja na kuzingatia mambo mbalimbali kabla ya kutoa majibu kwa mteja, mambo hayo ni pamoja na kusikiliza kuliko kuongea, kuheshimu mteja bila kujali hali au mahali alipotoka, kutoa majibu sahihi na yasiyo na ukakasi kwa mteja

Bi. Tibitha alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi hao kuwa kwa sasa wanahesabika katika kundi la watoa huduma lakini kesho watakuwa waomba huduma, hivyo wanatakiwa kutoa huduma wakiwa na dhana hiyo katika maisha yao ya utumishi wa umma.

Vile vile, Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Bi. Esther Mdegipala alisisitiza kuwa wateja wa ndani na wa nje wanakuja kuomba huduma wakiwa na matarajio yao hivyo watumishi wa umma wanatakiwa kuwa watulivu, wasikivu na kuelewa hoja aliyonayo mteja kisha kukidhi matarajio yake kwa mujibu wa taratibu na kanuni.

Pia, aliwaomba watumishi kutumia mifumo ya TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa kuwa mifumo hiyo inarahisisha kazi ya utoaji huduma kwa umma na inapunguza mianya ya rushwa.

Akihitimisha mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Utawala na Fedha Bw. Beyond Madege amesisitiza kuwa watumishi wa umma ni muhimu wakawa na taarifa sahihi za mteja ili kutoa huduma bora itakayomridhisha mteja huyo kwa Ustawi wa nchi.