Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WIKI YA HUDUMA KWA MTEJA KUONGEZA UWAJIBIKAJI KATIKA KUTOA HUDUMA BORA


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi ametoa wito kwa Watumishi wa Umma kuongeza uwajibikaji na kutoa huduma bora kwa Watumishi wa Umma kutoka katika taasisi mbalimbali, Wadau na Wananchi wanaohitaji kuhudumiwa kwenye masuala ya kiutumishi kwenye Wiki ya Huduma kwa Mteja iliyoanza tarehe 06 hadi 10 oktoba, 2025 yenye kaulimbiu isemayo 2025 Dhamira Inayowezekana.

Bw. Mkomi ametoa wito huo wakati akizungumza na watumishi wa ofisi yake katika eneo maalum la mafunzo kwa watumishi hao yanayofanyika kila siku ya Jumatatu Mtumba Jijini Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuimarisha utendaji kazi watumishi wa ofisi hiyo.

“Hii ni Wiki ya Huduma kwa Mteja, ninatoa wito kwa kila mtumishi kuwajibika katika eneo lake la kazi hasa mnapotoa huduma kwa Watumishi wa Umma wenzenu, Wadau na Wananchi hakikisheni mnatimiza malengo ya Serikali katika kutoa huduma bora kwa kila Mtanzania.” amesema Bw. Mkomi.

Kwa upande wake Mwezeshaji wa mafunzo ambaye ni Mratibu Msaidizi Utawala Bora, Ofisi ya Rais-IKULU, Bw. Andrew Massawe wakati akiwasilisha mada kuhusu Awamu ya 4 ya Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji 2023-2030 amesema malengo ya mkakati huo ni kuimarika kwa uwajibikaji na uwazi katika Taasisi za Umma na Taasisi zisizo za Kiserikali ikiwemo kutoa fafanuzi na elimu mbalimbali za kiutumishi katika jamii kwa ufasaha ili kutokuchafua taswira ya Utumishi wa Umma na kuwezesha jamii kushiriki kikamilifu katika juhudi za kukabiliana na Rushwa na kuimarisha Uadilifu.

Kadhalika, Bw. Massawe amesema, Watumishi wa Umma nchini wanategemea huduma za kiutumishi kutoka katika Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora hivyo huduma hiyo itolewe kwa uaminifu siyo tu katika Wiki ya Huduma kwa Mteja bali katika siku zote za utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo.