Habari
WAZIRI WA UTUMISHI ZANZIBAR, MHE. HAROUN ASISITIZA KUTUMIA BUSARA NA HEKIMA KATIKA USIMAMIZI WA RASILIMALIWATU

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman amesema kuwa uongozi ni kujitambua na ni dhamana, hivyo busara na hekima inatakiwa zaidi katika kufanya uamuzi ili kutoathiri utendaji kazi.
Waziri Haroun amesema hayo leo tarehe 13 Oktoba, 2023 wakati akifunga Kikao Kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kilichofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Jijini Arusha (AICC).
Mhe. Haroun amewasisitiza Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kuepuka kutumia nguvu katika usimamizi wa watumishi kwa kuwa hekima, busara, diplomasia na demokrasia zina matokeo chanya wakati wote wa kuongoza watu.
“Si kwamba sisi ni bora zaidi kuliko watumishi wengine lakini tumeaminiwa na Serikali na kupewa dhamana ya kusimamia watumishi wengine katika taasisi zetu. Hivyo, nawaomba kila mmoja atambue kuwa binadamu yeyote anataka kutambuliwa na kuheshimiwa wakati wote anapokuwa akitekeleza majukumu ya taasisi na Serikali kwa jumla” aliongeza.
Amesema ni imani yake kuwa katika kikao kazi hicho, washiriki wamepata nafasi ya kubadilishana uzoefu na kuelimishana kuhusu taratibu zinazopaswa kufuatwa katika kushughulikia masuala mbalimbali ya utawala na usimamizi wa rasilimaliwatu katika utumishi wa umma, hivyo watakaporudi katika vituo vyao vya kazi watatumia uzoefu huo kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa taratibu.
Naye, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi amesema kikao hicho kimejadili changamoto zinajitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya utawala na usimamizi wa rasilimaliwatu na namna bora ya kukabiliana nazo kwa pamoja.
Kikao kazi hicho cha siku tatu kimehitimishwa leo kwa kuweka maazimio mbalimbali ya kuboresha usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala katika utumishi wa umma.