Habari
MHE. RIDHIWANI KIKWETE ATEMBELEA TUME YA UTUMISHI WA UMMA, ATOA MAELEKEZO YA KUBORESHA UTENDAJI KWA USTAWI WA TAIFA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amefanya ziara ya kikazi Tume ya Utumishi wa umma na kutoa maelekezo mbalimbali ya kuboresha utendaji kwa ustawi wa taifa.
Mhe. Kikwete ametoa maelekezo hayo akiwa kwenye ziara yake ya kwanza katika Tume hiyo tangu alipoapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 18 Novemba, 2025 kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Pamoja na masuala mengine, Mhe. Kikwete ameilekeza Tume hiyo kuendelea kutenda haki katika kushughulikia Rufani na malalamiko ya Watumishi wa Umma na Mamlaka za Nidhamu. “Tutende haki, tusimame katika haki, lazima tuangalie katika utoaji haki, taratibu zizingatiwe, uchunguzi wa kina ufanyike kabla ya kumchukulia mtumishimi hatua,” amesisitiza Mhe. Kikwete.
Pia ameitaka Tume hiyo kuendelea kutoa nafasi kwa Warufani na Warufaniwa kufika na kusikilizwa mbele ya Tume kwa ajili ya kutoa ushahidi zaidi.
Mhe. Kikwete ameisisitiza Tume kuendelea kutoa Miongozo ya masuala ya Ajira na Nidhamu ambayo husaidia kuwa na tafsiri sahihi ya utekelezaji wa sheria katika Utumishi wa Umma.
Aidha, ameielekeza Tume hiyo kuendelea kufanya ukaguzi wa masuala ya Rasilimaliwatu na uzingatiaji wa Sheria katika Taasisi za Umma hususani kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma ili kuhakikisha Watumishi wa Umma wanapata haki zao kuanzia wanapoajiriwa hadi wanapostaafu.
Mhe. Kikwete ametoa wito kwa Tume hiyo kuwashauri waajiri kuweka mazingira wezeshi ya kufanya kazi (vitendea kazi, maslahi na miundo mbinu sahihi ya kufanya kazi) na kuhakikisha uwepo wa Mabaraza ya Wafanyakazi yaliyo hai na yanafanya kazi kwa mujibu wa Sheria.
