Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WAZIRI KIKWETE AWATAKA TPSC KUFANYA TAFITI ZITAKAZOSAIDIA KUBORESHA UTUMISHI WA UMMA NCHINI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameitaka Menejimenti ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kufanya tafiti zitakazosaidia kuboresha Utumishi wa Umma nchini kwa ustawi wa taifa.

Mhe. Kikwete ameyasema hayo leo tarehe 27 Novemba, 2025 alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) wakati wa ziara yake ya kikazi katika Chuo hicho jijini Dar es Salaam.

Amesema ni jukumu la TPSC kueleza ukweli kwa kufanya tafiti, kwani wanao wajibu wa kuhakikisha Utumishi wa Umma unakaa vizuri, “tuambieni yale mnayofikiri ni vema yakafanyika ili kuwa na Utumishi wa Umma bora, hatuwezi kufanikiwa kama Chuo hiki kitashindwa kutuambia wapi kuna tatizo,” amesisitiza.

“Tufanye tafiti tujiulize, kuna vitu gani tunatakiwa kuviboresha, lazima tujadili Utumishi wa Umma kwa upana wake. Huwezi kuwa Mtumishi wa Umma na matendo yako hayafanani na Utumishi wa Umma Mhe. Kikwete amesema.

Aidha, Mhe. Kikwete ameipongeza taasisi hiyo kwa kufanya kazi nzuri na kuisisitiza kuendelea kutoa mafunzo elekezi na kujitangaza zaidi ili Chuo hicho kifahamike kwa wananchi na kutoa fursa ya kujiunga huku akiwataka kujielekeze zaidi kwenye Dira waka ya Maendeleo ya Taifa 2050 katika utekelezaji wa majukumu yao.

Ameitaka taasisi hiyo kumshirikisha pale wanapokwama kutekeleza majukumu yao ili aone namna ya kuwezesha. “Nishirikisheni pale mnapokwana ili tusaidiane namna bora ya kufanya, kwangu hakuna jibu la hapana, kuna haiwezekani lakini tukifanya hivi itawezekana. Tupeane ushirikiano mkubwa kwani ndio utakaotusaidia kusonga mbele.” Mhe. Kikwete ameongeza.

Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu-UTUMISHI, Bw. Nolasco Kipanda amesema Katibu Mkuu-UTUMISHI anafurahia kuona Waziri Kikwete akifanya ziara katika taasisi zilizo chini ya Ofisi yake, kwani anaamini anaweka msingi katika maeneo mbalimbali ya kuboresha utendaji.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Mkuu wa Chuo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Ernest Mabonesho ametoa shukrani kwa Waziri Kikwete kwa kutenga muda wake na kuwatembelea katika chuo chao na kuahidi ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.