Habari
WAZIRI KIKWETE AMTEMBELEA MAMA SALMA OMAR ALI JUMA NA MAMA REGINA LOWASSA
Na. Antonia Mbwambo na Veronica Mwafisi-Dar es salaam
Tarehe 22 Januari, 2026
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewatembelea na kuwajulia hali Mama Salma Omar Ali Juma, Mjane wa Hayati Dkt. Omar Ali Juma, Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nyumbani kwake Msasani jijini Dar es Salaam na Mama Regina Lowassa, Mjane wa Hayati Edward Ngoyai Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nyumbani kwake Masaki Jijini Dar es Salaam leo Januari 22, 2026.
Mhe. Kikwete amesema, Ofisi ya Rais-UTUMISHI inazingatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuthamini mchango wa Viongozi Wakuu wa Kitaifa Wastaafu pamoja na wajane wa Viongozi hao Wastaafu ikiwa ni pamoja na kuwatunza kwa mujibu wa Sheria.
“Mhe. Rais yupo pamoja nanyi na amenielekeza kufikisha salamu zake kwenu kwa kuwajulia hali, kusikiliza changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi kwa kuwa anathamni mchango wa Viongozi Wakuu wa Kitaifa Wastaafu pamoja na wenza wa Viongozi hao” amesema Mhe. Kikwete
Kwa upande wake, Mama Regina Lowassa, Mjane wa Hayati Edward Ngoyai Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemshukuru na kumpongeza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuijali familia ya Hayati Edward Lowassa wakati wote bila kuchoka.
“Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa pamoja nasi wakati wote, nitoe shukrani kwa niaba ya familia kwa hekima na busara ambazo mnatumia katika kutuhudumia Wenza wa Viongozi Wakuu wa Kitaifa Wastaafu,”Amesema Mama Lowassa
Aidha, Mama Salma Omar Ali Juma, Mjane wa Hayati Dkt. Omar Ali Juma, Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemshukuru Mhe. Kikwete kwa kupata nafasi ya kumtembelea na kumjulia hali na kumuomba amfikishie salamu za shukrani Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufuatilia kwa karibu masuala yanayowahusu na kuyatafutia ufumbuzi kupitia Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora.
