Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATUMISHI WATAKIWA KUWA NA NIDHAMU YA MATUMIZI YA FEDHA BINAFSI


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Juma Mkomi amewasihi watumishi wa ofisi yake kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha binafsi kwa kuwa huonesha tabia ya mtu haraka katika jamii.

Bw. Mkomi alisema hayo Novemba 24, 2025 wakati alipokuwa akiongea na watumishi wa ofisi yake mara baada ya kupata mafunzo ya usimamizi wa fedha binafsi yaliyotolewa na Mtoa Elimu wa Masuala ya Fedha (CFE) Bw. Edmund Munyagi katika Ofisi za Utumishi zilizopo Mtumba jijini Dodoma.

“Natoa rai kwa kila mtumishi wa ofisi hii kuhakikisha anajitahidi kudhibiti matumizi ya fedha binafsi ili yasizidi kipato na kutumia akiba inayobaki katika matumizi muhimu kuwekeza katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja kwa manufaa baadae” alisema Bw. Mkomi.

Aliongeza kuwa wataalamu wa fedha wanasisitiza kuwekeza katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja ili kukuza vipato na ni njia bora ya kukuza mtaji wa mtu binafsi kwa kutumia njia za kitaalamu.

Naye, Mtoa Elimu ya Masuala ya Fedha (CFE) Bw. Edmund Munyagi alibainisha kuwa tabia ya binadamu imejificha sana ingawa, fedha inaweza kuonesha tabia ya mtu kwa haraka.

“Ukitaka kujua tabia ya mtu haraka apate fedha ili aonekane namna anavyoitumia na jamii nzima itatambua kuwa mtu fulani amepata fedha” alisema Bw. Munyangi.

Pia, alisema kuwa Mifuko ya uwekezaji wa pamoja hukusanya fedha kutoka kwa wawekezaji wengi na kuziwekeza kwenye hisa, dhamana, au mali nyingine ili kupunguza hatari ya kupotea na kuongeza faida kwa wawekezaji.

Ofisi ya Rais UTUMISHI imeweka utaratibu wa kutoa mafunzo mbalimbali kila siku ya Jumatatu kwa watumishi wake  ili kuboresha utendaji kazi.