Habari
WATUMISHI WATAKIWA KUJENGA IMANI KWA WANANCHI

“Wananchi wanaimani na utendaji wa Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, hivyo hakuna budi kuilinda imani hiyo kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa umma”.
Maneno hayo yamesemwa Bw. Paul Mashauri ambaye ni Mchumi na Mjasiliamali, Septemba 29, 2025 wakati akitoa mafunzo ya namna bora ya kuboresha utendaji wa Watumishi wa umma yaliyofanyika katika Jengo la Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Mtumba Jijini Dodoma.
Aliongeza kuwa, kila mwananchi anatamani kupata huduma bora haraka na kwa wakati, hivyo watumishi wanatakiwa kuwathamini wananchi na kuwapa huduma wanayohitaji ndani ya muda mfupi ili kuongeza imani kwa Serikali.
“Ni kazi ya Watumishi wa Umma kutafsiri Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kutoa huduma bora kwa wananchi. Wananchi hawawezi kusoma nyaraka za mipango ya maendeleo ya nchi kwa upana wake isipokuwa ni jukumu la watumishi na wananchi wanataka kuona huduma bora tu” alifafanua Bw. Mashauri.
Kwa upande mwingine, Mtaalamu wa Epidemiolojia sehemu ya Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya Bw.Jofrey Mtewele aliwataka watumishi hao kuepuka visababishi na kuwa makini na magonjwa yasiyoambukiza kwa kuwa hapa Tanzania yanachangia vifo kwa asilimia 33.
Bw. Mtewele alitaja baadhi ya magonjwa hayo kuwa ni saratani, kisukari, ugonjwa wa mifumo ya upumuaji, moyo na mishipa ya damu.
Naye, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bw. Syrus Kapinga amewashukuru wawezeshaji hao Bw. Mashauri na Bw. Mtewele kwa kutoa mafunzo muafaka kwa watumishi wa ofisi hiyo na kuwaahidi kutekeleza kwa vitendo mafunzo hayo.
Aidha, Bw. Kapinga ametoa rai kwa watumishi wote kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara kwa kuwa magonjwa yaliyotajwa na wataalamu yapo na yanaweza kutibika.
Vilevile, Bw. Kapinga ametumia fursa hiyo kuwapongeza watumishi wa ofisi yake waliozaliwa mwezi Septemba na kuwatakia kila kheri katika maisha yao.