Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATUMISHI WA UMMA WASISITIZWA KUSHUGHULIKIA MREJESHO WA WANANCHI KWA HAKI NA KWA WAKATI


Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Felister Shuli amewasisitiza Watumishi wa Umma kushughulikia kwa haki na kwa wakati mrejesho unaowasilishwa na wananchi kupitia Mfumo wa (e- Mrejesho) ili kujenga imani na heshima ya Serikali kwa umma.

Bi. Shuli ameyasema hayo leo Aprili 21, 2026 wakati akimuwakilisha Katibu Mkuu-UTUMISHI Bw. Juma Mkomi katika ufunguzi wa mafunzo ya matumizi ya kutuma, kupokea na kufuatilia malalamiko, mapendekezo, maulizo na pongezi kwa watumishi kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Taasisi zilizo chini yake.

“Ili kufikia utumishi wa umma unaowajibika na uliotukuka, ni vizuri tukashughulikia mrejesho wa wananchi kwa haki na uharaka zaidi.” Bi Shuli alisema.

Amesema, Watumishi wa Umma wanapaswa kuwa na mabadiliko katika fikra, mitazamo, mifumo na tabia walizonazo ili kuwa na Utumishi wa Umma wenye matokeo chanya na thamani halisi kwa mwananchi.

Bi Shuli ameongeza kuwa uzingatiaji wa maadili katika utumishi wa umma si kuzifuata tu Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma bali ni pamoja na kuutumia ipasavyo utaalamu unaohusu ushughulikiaji wa mrejesho wa wananchi .

Amesema ni jukumu la kila mshiriki kuonesha ushirikiano na kuzingatia utu hususani wanapotoa huduma kwa wateja pamoja na kuwa waaminifu hasa katika utunzaji siri kwa kuwa kazi watakazofanya zitahitaji kuwa na matumizi sahihi ya taarifa.

Aidha, amewapongeza washiriki wote kwa kuhudhuria mafunzo hayo na kuwataka wajifunze kwa bidii ili wawe wataalamu watakaowajibika kikamilifu

Kwa upande wake mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Afisa TEHAMA kutoka Watumishi Housing Investiments (WHI) Bw. Albano Lukiano   amemshukuru Bi. Shuli kwa kuwafungulia mafunzo hayo na kuahidi kuwa yale yote watakayofundishwa watayazingatia na kuyafanyia kazi ili kutoa huduma bora kwa manufaa ya umma.