Habari
WATUMISHI WA UMMA WASISITIZWA KULINDA AFYA ZAO
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Juma Mkomi ametoa rai kwa kila mtumishi wa umma kuhakikisha analinda afya ya mwili na akili kuanzia nyumbani kwa kuwa mtumishi mwenye afya njema anakuwa na uwezo wa kufikiri na kufanya uamuzi sahihi katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Juma Mkomi wakati akiongoza kikao cha kuchagua mfanyakazi bora wa Ofisi yake kilichofanyika Aprili 13, 2026 katika ofisi hiyo Mtumba Jijini Dodoma.
Bw. Mkomi aliongeza kuwa, watumishi wanapaswa kujenga utamaduni wa kujali afya zao kwa kuzingatia lishe bora, kufanya mazoezi ya mwili pamoja na kupata muda wa kupumzika ambapo masuala yote hayo huanzia katika mazingira ya nyumbani.
Watumishi wa umma wanapokuwa na afya dhaifu, utendaji kazi hushuka na hivyo kuathiri moja kwa moja utendaji kazi mahala pa kazi. Hivyo amewakumbusha watumishi hao kuwa afya njema ni msingi imara katika utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi.
Aidha, Katibu Mkuu huyo ametumia fursa ya kikao hicho kuitakia kila la kheri Utumishi Sports Club ambayo inaelekea kwenye mashindano ya Mei Mosi yatakayofanyika mkoani Njombe.
Bw. Mkomi amewahimiza wachezaji pamoja na benchi la ufundi kujituma, kudumisha nidhamu na kuzingatia maadili ya michezo ili kuiwakilisha vyema ofisi.
“Nendeni kwenye mashindano hayo muhimu na onesheni nidhamu njema na kiwango bora zaidi cha ushindani ukilinganisha na kiwango mlichoonesha wakati wa mashindano ya SHIMIWI 2025. Zingatieni nidhamu, mshikamano na ushirikiano ili kuendelea kuleta ushindi katika ofisi yetu” alisisitiza Bw. Mkomi.
