Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATUMISHI WA UMMA WAKUMBUSHWA KUZINGATIA MAADILI KATIKA UTENDAJI KAZI ILI KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI


 

Na Antonia mbwambo-Iringa

Tarehe 27 Novemba,2025

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray ametoa wito kwa Watumishi wa Umma nchini kuzingatia maadili ya utendaji katika utekelezaji wa majukumu yao ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Qwaray ameyasema hayo leo tarehe 27 Novemba, 2025 wakati akifungua kikao kazi kilichoshirikisha Maafisa Rasilimaliwatu na Maafisa Sheria kutoka taasisi za Serikali kwa lengo la kubadilishana uzoefu kuhusu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa Sheria namba 298 ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.

“Watumishi wa Umma mzingatie maadili na kufuata Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria ili kuondokana na changamoto katika utoaji wa huduma bila kujali unayemhudumia unamfahamu au haumfahamu kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi kwa manufaa ya Umma.

Aidha Mhe, Qwaray amesisitiza kwamba, kila Mtumishi wa Umma ana wajibu wa kuepusha migogoro na malalamiko mahali pa kazi lakini pia kuutendea haki muda waliopewa na serikali katika kuhudumia wananchi.

Vilevile, Naibu Waziri Qwaray ametoa wito kwa watumishi wa Umma kutumia rasilimali zilizopo ipasavyo kwa kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na kwa wakati na kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Awali, akitoa neno la utangulizi, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Bi. Hilda Kabissa amesema kikao kazi hicho kimelenga kuchambua utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma ili kuimarisha utendaji kazi na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kwa Upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu ambaye ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Bi Felista Shuli wakati akimkaribisha Naibu Waziri kufungua kikao kazi hicho amesema kumekuwa na ukiukwaji wa Kanuni, Miongozo, Taratibu na Nyaraka mbalimbali zinazoandaliwa kwa ajili ya kuwapa mwongozo  Watumishi wa Umma hivyo, kupitia kikao kazi hicho kitawezesha Watumishi kuwa na uelewa juu ya Sheria na Kanuni hizo kwa lengo la kuongeza uwajibikaji wenye tija.