Habari
WATUMISHI WA UMMA NCHINI WAASWA KUACHA KUKOPA KUPITA KIASI

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Ofisi Rais, UTUMISHI, Bi.Felister Shuli amewaasa Watumishi wa Umma nchini kuacha tabia ya kukopa kupita kiasi huku akisisitiza kuwa kitendo hicho ni kinyume na maadili katika Utumishi wa Umma nchini.
Mkurugenzi Shuli ametoa kauli hiyo leo Jumanne Agosti 26, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha mada ya Maadili katika Utumishi wa Umma katika Mkutano wa 13 wa Chama Cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka ( TRAMPA) unaotarajiwa kufunguliwa rasmi kesho na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa.
Amesema kitendo hicho cha Mtumishi kukopa kupita kiasi humpelekea kupata msongo wa mawazo na kusababisha kuwahudumia wateja kwa ukali au kwa kukosa staha kutokana msongo wa mawazo alionao unaosababishwa na madeni
Ameongeza kuwa baadhi ya Watumishi waliokopa kupita kiasi hujikuta ni watu wa kuhangaika hangaika na muda mwingine huwa na mahudhurio hafifu kazini " huwa ni watu wa kujificha na kukimbia kimbia ili wadai wake wasiweze kuwaona kwani baadhi ya wadai wao huwafuata ofisini" amesema
Kufuatia hatua hiyo, Bi.Shuli amewataka Watumishi kuishi kulingana na kipato chao ili wasiweze kujiingiza kwenye madeni yasiyolipika na hivyo kusababisha kushindwa kutoa huduma bora kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Bi.Shuli amewataka watumishi wa umma kujiepusha na michezo ya bahati nasibu na kubashiri ( betting ) kwani ni ukiukwaji wa Maadili katika Utumishi wa Umma nchini
" Jiepusheni na "betting" kwani watumishi wanaocheza michezo hiyo hujikuta wakitumia muda mwingi na fedha nyingi kucheza michezo hiyo na hivyo kusababisha kukopa kupita kiasi.