Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATUMISHI WA OFISI YA RAIS - UTUMISHI WAPATIWA MAFUNZO JUU YA KUJITAMBUA


Watumishi wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, leo Septemba 1, 2025 katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma wamepatiwa mafunzo ya kujitambua kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.

Akizungumza baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Bw. Cyrus Kapinga ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera amesema kuwa kujitambua ni msingi wa kila mtumishi kujua nafasi yake, uwezo wake na wajibu wake katika kuwahudumia wananchi kwa weledi na uadilifu.

Mafunzo hayo ambayo hufanyika kila Jumatatu ya wiki yameelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa ofisi hiyo kuboresha utendaji kazi na kuwajengea uwezo watumishi wa umma katika maeneo ya mawasiliano, uongozi, ubunifu na uwajibikaji.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo Bi. Noela Bomani ameeleza kuwa kujitambua sio nguzo muhimu ya mafanikio ya mtu binafsi tu, bali ni ya taasisi, kwani humsaidia mtumishi wa umma kutambua nguvu na udhaifu wake, hivyo kuwezesha kufanya maamuzi sahihi ya kikazi na kijamii.

Mafunzo hayo yametoa msisitizo katika maeneo ya mawasiliano chanya, nidhamu ya kazi, kujenga mshikamano wa kikazi, ushirikiano ikiwa pamoja na kukuza thamani ya Taifa na utu. Aidha, watumishi wametakiwa kutumia uelewa walioupata ili kuongeza ari ya kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.