Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATUMISHI OFISI YA RAIS - UTUMISHI WASISITIZWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA.


Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathimni Ofisi ya Rais – UTUMISHI Bw. Patrick Allute kwa niaba ya Katibu Mkuu leo Disemba 22, 2025 amewasisitizwa watumishi wa ofisi hiyo kuongeza bidii katika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na viwango vya maadili ya Utumishi wa Umma ili kuimarisha ufanisi katika utoaji huduma kwa wananchi.

Bw. Allute alisema hayo kwa Watumishi wa Ofisi hiyo wakati wa Mafunzo ya kuwajengea watumishi uwezo wa kiutendaji ambayo hufanyika kila jumatatu ya wiki katika eneo maalum la Ofisi hiyo lililopo Mtumba jijini Dodoma.

“Ni wajibu wa kila mtumishi kuhakikisha anazingatia kanuni za maadili ya Utumishi wa Umma kwa kutenda haki, kuwa mwaminifu, pamoja na kuepuka vitendo vya rushwa au matumizi mabaya ya madaraka.” Bw. Allute alisema

Aidha, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya ukuzaji maadili Bw. Ally Ngowo amesema watumishi wanatakiwa kuendelea kuheshimu muda wa kazi, kudumisha siri za serikali, pamoja na kuweka mbele ustawi wa wananchi katika majukumu yao ya kila siku.

“Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi na tathmini ya utendaji kazi ili kuhakikisha rasilimali za umma zinalindwa na kutumika ipasavyo kwa maslahi ya Taifa.”

Kwa upande wao, baadhi ya watumishi wa Ofisi hiyo wameeleza kuwa mafunzo ya mara kwa mara kuhusu maadili na utendaji yanaongeza uelewa na kuimarisha ufanisi wao, na kuahidi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu