Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATUMISHI OFISI YA RAIS-UTUMISHI WAKUMBUSHWA KUZINGATIA KANUNI ZA MAADILI YA UTENDAJI KATIKA UTUMISHI WA UMMA.


Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wamekumbushwa juu ya kuzingatia Kanuni za Maadili zinazowaongoza katika utendaji wao kwa kufuata Sera, Sheria na Taratibu zilizopo ili kuleta tija kwa maslahi mapana ya Taifa.

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais - UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Musa Magufuli ameyasema hayo leo tarehe 15/09/2025 alipokuwa akizungumza na watumishi wa Ofisi hiyo iliyopo Mtumba jijini Dodoma baada ya mwezeshaji kuhitimisha mafunzo ambayo hufanyika mwanzoni mwa kila wiki.

Bw. Magufuli amesema,ni vyema watumishi  kuwajibika kwa umma kwa kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora na kwa wakati bila kujali uhusiano uliopo kati ya mtumishi na mwananchi anayepewa huduma.

Awali, akitoa mafunzo hayo, Afisa Habari Mkuu Idara ya Usimamizi wa Maadili, Ofisi ya Rais, UTUMISHI Bw. Rocky Setembo amesema, Kanuni hizo ndizo zinazomuongoza mtumishi juu ya tabia na mwenendo mwema  wa kuzingatia ili kuleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma.

Bw. Setembo ameongeza kuwa, kwa kufuata kanuni hizo kutamuwezesha mtumishi wa umma kuepuka viashiria vyovyote vitakavyosababisha uvunjifu wa amani na kuwa mfano bora wa kuigwa katika jamii inayomzunguka.